September 30, 2013





Na Saleh Ally
Gumzo la mshambuliaji Mrisho Ngassa kuhamia katika kikosi cha Yanga huenda lilikuwa kubwa zaidi wiki iliyopita kwa kuwa alikuwa amemaliza kipande cha adhabu yake ambayo ilikuwa ni kufungiwa mechi sita na baadaye kulipa Sh milioni 45 kwa Klabu ya Simba.


Klabu ya Simba ilimsajili Ngassa, akaichezea timu hiyo na wakaongeza mkataba kabla ya yeye kuamua kujiunga na Yanga. Ilipopitishwa adhabu ya kutocheza mechi sita na kulipa fedha hizo, Yanga ilikata rufaa lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likajikausha hadi mwisho.

Alipomaliza adhabu ya mechi sita, msisitizo wa shirikisho hilo ulikuwa ni Ngassa kulipa fedha hizo ndiyo aanze kucheza. Ndiyo maana gumzo likaibuka upya lakini siku moja kabla ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Ngassa akatua TFF na kukabidhi fedha hizo za Simba.

Ishu kwa mashabiki wa Yanga zilikuwa mbili. Kwanza kusikia Ngassa analipa deni hilo na baada ya hapo kumuona akiwa uwanjani anaitumikia timu yake katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.



Kwetu (Gazeti la Championi), tulikuwa na uhakika kuwa Ngassa atacheza. Tulikuwa na listi kamili, hadi Ngassa atacheza namba ipi, ilianikwa kwenye ukurasa wa mbele kabisa.

Mashabiki wengi walikwenda uwanjani huenda kuhakikisha kama kweli Championi lilikuwa na uhakika, hilo walilihakikisha. Lakini pia walitaka kukiona kikosi chao kikiwa na Ngassa baada ya zaidi ya misimu mitatu tangu alipoondoka na kujiunga na Azam FC kwa uhamisho wa Sh milioni 98.


Ngassa alikuwa amerejea kwa mara ya kwanza na kuichezea Yanga katika mechi ya mashindano. Matumaini kwake kutoka kwa mashabiki yalikuwa juu na wengi waliamini atafanya vizuri sana.
Hakika hakucheza katika kiwango cha juu sana kama ambavyo wengi walitegemea, alijitahidi lakini bado si Ngassa yule mwenye uwezo wake unaofahamika.

Ilionekana kabisa kwamba kiasi fulani mechi ilikuwa ngumu kwake na mambo kadhaa yalichangia, moja likiwa ni uchezaji wa ‘kazikazi’ wa wanajeshi wa Ruvu Shooting ambao ulimtatiza karibu kila mchezaji wa Yanga.

Lakini suala la mfumo au alivyotumika huenda pia lilikuwa tatizo, mara kadhaa alilazimika kuingia na kucheza ndani lakini kukawa hakuna mipira mirefu.

Inaonekana wazi kuna tatizo la uchezaji kati ya kiungo cha Yanga na Ngassa. Anapokuwa akicheza pembeni au katikati, anahitaji kiungo mwenye haraka zaidi kutoa pasi badala ya madoido.

Kipindi cha kwanza:
Mashabiki walionekana kuwa na uhakika wa Yanga kufanya vizuri katika mechi hiyo kwa kuwa katika kikosi cha wachezaji 11, ndani yake kuna Ngassa.
Kweli alianza vizuri kipindi cha kwanza, alifanikiwa kupiga pasi 20, kati ya hizo akapoteza nne, maana yake 16 ndiyo zilifika. Akapiga krosi tatu.

Walinzi na viungo wa Ruvu Shooting walimchezea faulo nne katika kipindi hicho cha kwanza na akaonekana ni msumbufu katika ngome yao.

Kipindi cha pili:
Katika kipindi hiki alipiga pasi 14, akapoteza nne pia na akachezewa faulo nne tena kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza.
Ngassa alipiga krosi nne na moja ndiyo ilizaa bao lililofungwa na Hamis Kiiza. Alipata mpira kutoka kwa Haruna Niyonzima, haraka akaongeza kasi na kumpita beki Stephano Mwasyika kabla ya kupiga krosi safi.
Ukiangalia jumla alipiga pasi 34, akapoteza nane na jumla ya krosi saba kwa vipindi vyote.

Bado:
Kwa takwimu hizo, kwa uchezaji wa Ngassa, maana yake alicheza kwa kiwango cha chini, kwa uwezo wake anaweza kucheza zaidi.
Inawezekana kabisa mfumo unampa shida kwa kuwa hiyo ni mechi ya kwanza chini ya Ernie Brandts na Mholanzi huyo anapaswa kuliangalia hilo.
Upande wake Ngassa, pia anapaswa kuongeza juhudi zaidi kwa kuwa jicho la wengi liko kwake kwa maana ya tegemeo.
Tatizo moja ambalo linaweza kushughulikiwa na kurudisha makali ya mshambuliaji huyo ni wepesi wa viungo. Niyonzima ni mmoja wa viungo bora lakini si mwepesi kuachia mpira kwa haraka.
Muda mwingi anazunguka nao, uchezaji wa Ngassa unahitaji mtu mwenye kasi na mwepesi wa kuachia.  Mfano mzuri unaweza kuwa ule wa Athumani Idd ‘Chuji’ ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Alimpa Ngassa zaidi ya pasi sita za haraka na mabadiliko yakaonekana. Chuji ni mwepesi kidogo kuachia mipira na ndiye kiungo mwenye uwezo wa kupiga pasi ndefu kuliko wote katika Ligi Kuu Bara.
Mwisho kwa dakika 90 alizocheza Ngassa, zimewafundisha jambo mashabiki kwamba muhimu ni timu na si mtu. Hivyo wanachotakiwa ni kuamini kikosi kizima.
FIN.






0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic