September 18, 2013




Mmoja wa wasomaji wa gazeti hili ambaye amekuwa rafiki yangu kutokana na kutoa maoni mara kadhaa, wakati mwingine akikosoa au kusifia, aliniandikia ujumbe mfupi ambao ulisababisha nimuonee huruma.


Aliniambia amenyimwa visa ya kuingia nchini Uswiss, lengo lake lilikuwa ni kwenda kufanya kazi lakini hataweza kuipata kwa kuwa amenyimwa viza na anachoamini ni kutokana na mfululizo wa vijana wa Kitanzania kukamatwa na madawa ya kulevya katika mipaka ya nchi mbalimbali.

Inawezekana kukataliwa kwake kukawa hakujaunganishwa na suala hilo la Watanzania kukamatwa mfululizo wakiwa wamebeba unga, lakini ninaona ana haki ya kufikiria hivyo kwa kuwa ni mambo yanayoweza kuendana.
Sakata la vijana wa Kitanzania kukatwa mfululizo limekuwa likipanda mfululizo na limeingia kwenye sanaa na sasa michezo.
Kuna wasanii wanashikiliwa nchini Afrika Kusini lakini siku chache tumeona mambo yamehamiwa kwa wanamichezo. Taarifa za kukamatwa kwa mwanasoka Joseph Kaniki aliyewahi  kuichezea hadi timu ya taifa, Taifa Stars.

Kaniki amekamatwa akiwa na Mkwanda Matumla, bondia kutoka familia ya Matumla na imeelezwa kaka yake, Mbwana naye amekamatwa barani Ulaya pia akiwa amebeba madawa. Hii si hali nzuri na hakika kuna kitu cha kufanya.

Serikali ina mkono mrefu na kila mmoja analitambua hilo, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuamua kupambana na kulimaliza suala hili ili kuikoa jamii yetu kwa kuwa tuendako tunapanda mmea wa matatizo utakaoangamiza kabisa taifa letu.

Takwimu zinaonyesha Marekani ndiyo nchini inayoongoza kwa kuwa na vichaa wengi duniani, nchi nyingine za Amerika Kaskazini kama Venezuale zinaingia katika hilo na moja ya tatizo ni suala la madawa za kulevya.
Tanzania nib ado nchi changa, haitaweza kujikwamua katika kipindi kifupi kama nguvu kazi ya taifa ambao ni vijana watakuwa wakiishi katika maisha hayo haramu, kila kukicha wanakamatwa katika nchi za watu.

Hasara ni nyingi kwa taifa, lakini hizi mbili nguvu kazi ya taifa kuteketea na madawa ya kulevya, iwe kwa kutumia au kukamatwa si jambo jema na inabidi lifanyiwe kazi, ikibidi serikali iamshe kampeni maalum kuhakikisha inapita katika mirija inayotumika.

Pili ni sifa ya nchi yetu, yule msomaji wa Championi aliyenitumia ujumbe, sasa amekosa kazi na bado ninaamini kwamba tatizo hilo linaweza kuwa sehemu ya tatizo lake. Kama halitakuwa tatizo, jina la nchi yetu linachafuka.

Watanzania wanaosafiri katika nchi mbalimbali wanaweza kuwa watu watakaoelezea ugumu wa mambo ulivyo kwa sasa katika kila mpaka au uwanja wa ndege katika nchi za wenzetu unaposema wewe ni Mtanzania, hakuna anayekufurahia na kila mmoja anakuwa na hofu kubwa nawe.

Watanzania wanakaguliwa sana na hawaamini tena, tumeanza kuonekana ni kama taifa fulani la matapeli au wakosaji. Lakini kumbukeni sifa yetu ni amani na watu waungwana, serikali isikae kimya wakati suala hilo linaharibika.
Wanasema kinga ni bora kuliko tiba, serikali haipaswi kusubiri kesho au jioni, yaani mambo yakiwa yameharibika zaidi ili ianze kutafuta tiba ya suala hilo, sasa ndiyo wakati mwafaka na hakuna linaloshindikana kama serikali itaamua kupambana.
Mambo yatakuwa magumu pale tu serikali watakapoona suala hili halina sababu ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na mwisho kukata mirija inayotumika kuwaingiza vijana, hasa wale wenye tamaa na maisha ya haraka katika mlolongo huo.
Tamaa ya maisha mazuri ya haraka, uvivu na kukosa uvumilivu ni sehemu ya haya yanayotokea vijana kutumika kama ‘posta’ ya usafirishaji madawa ya kulevya. Serikali nimeiomba iingie, lakini vijana wenzangu nawashauri kutafakari mara mbili, kwamba maisha mazuri yanaweza kupatikana bila ya kubeba unga na kujiingiza hatarini huku wanaotajirika zaidi ni wale waliokaa kando na wanaingiza faida nyingi zaidi. Amkeni.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic