NA TFF
Mamlaka za Mkoa wa Mwanza zimesema
zitatimiza ahadi yao ya kuchangia dola 118,000 za Marekani (zaidi ya sh.
milioni 190) ili kukamilisha mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa
Nyamagana, jijini Mwanza kabla ya Oktoba 15 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza,
Mhandisi Evarist Ndikilo pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus
Mabula wametoa ahadi hiyo wakati wa kikao kati yao na Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga kilichofanyika leo (Septemba 25
mwaka huu) kwenye ofisi za TFF.
Wakuu hao wa Mwanza katika kikao
hicho pia walifuatana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.
TFF ilipeleka mradi wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Goal Project IV wa nyasi bandia wa dola
500,000 za Marekani katika Uwanja wa Nyamagana.
Mradi huo ulipelekwa huko baada ya
Mkoa wa Mwanza kuahidi kuchangia dola 118,000 ili kukamilisha thamani ya mradi
mzima ambayo ni dola 618,000 za Marekani. Wamiliki wa uwanja huo ni Jiji la
Mwanza.
Goal Project I ilitumika kwa ajili
ya ujenzi wa hosteli ya TFF (technical centre), Goal Project II nyasi bandia
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume wakati Goal Project III iliweka nyasi bandia
katika Uwanja wa Gombani ulioko Pemba, Zanzibar.
Captions:
Rais wa TFF, Leodegar Tenga (wa pili kushoto) akiwa na ujumbe wa Mkoa wa Mwanza
ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo ulipomtembelea katika
ofisi za TFF jana. Wa tatu kutoka kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,
Stanslaus Mabula akifuatiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.








0 COMMENTS:
Post a Comment