September 30, 2013




Na Saleh Ally
Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusiana na ipi hasa ni ligi ngumu zaidi kati ya zile kubwa nne za Ulaya.

Ligi kubwa nne za Ulaya chini ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) ni Ujerumani, maarufu kama Bundesliga, Hispania (La Liga), England (Premiership) na Italia (Serie A).


Wakati fulani, Waingereza wamewahi kusisitiza ligi yao ni ngumu zaidi lakini Hispania na hata Wajerumani wamekuwa wakipinga hilo.

Achana na takwimu za michuano iliyo chini ya Uefa, kama utakwenda kwa ligi husika, kumekuwa na ushindani mkubwa sana kati ya Premiership na Bundesliga kutokana na mwenendo na vigezo kadhaa.
Achana na msimu uliopita ambao Bundesliga iliongoza katika vitu vingi sana, msimu huu mambo yanaonekana kuwa tofauti kidogo na huenda England ikashinda nafasi ya juu zaidi hadi msimu utakapomalizika.
Katika ligi zote, kila upande umecheza zaidi ya mechi 50, takwimu zinaonyesha England ndiyo kugumu zaidi na mashabiki wanaingia kwa wingi zaidi hata kuliko Ujerumani.

Ushindani, kiasi cha karibu kila timu kutokuwa na uhakika wa kushinda mechi yoyote, unawavutia mashabiki hao kwa kuwa katika mechi sita tu ambazo kila timu imecheza kabla ya wikiendi, tayari kila moja ilikuwa imepoteza mechi moja bila ya kuangalia hii ni Manchester United, Chelsea au Arsenal.

Ujerumani inaporomoka haraka kwa idadi ya watazamaji, huenda tabia ya mechi kali kuwa ni zile zinazohusisha timu kubwa tu kama Bayern Munich na Borussia Dortmund, basi. Na Hispania pia mambo ni yaleyale tu, kwani ushindani unaonekana zaidi kwa Real Madrid na Barcelona.

England kila mechi haina mwenyewe, kila upande ‘unakaza’ kuepuka aibu ya kipigo na ushindi unahesabika kila baada ya dakika 90.
Angalia baadhi ya vigezo vinavyoonyesha kama Premiership itakwenda kwa wastani mzuri ilioanza nao, basi ndiyo itakuwa ligi ngumu zaidi hadi mwisho wa msimu.

Wingi wa watazamaji:
Kwa misimu mitatu mfululizo, Ujerumani wamekuwa wakiongoza kwa wingi wa watazamaji ambao wameingia viwanjani.
Lakini katika mechi 50 zilizopita, England inaongoza kwa kuwa na wastani mkubwa wa watazamaji walioingia uwanjani.

Wastani wa ukubwa wa viwanja vyote ni 36,622 lakini wastani wa watazamaji walioingia kwenye mechi 50 zilizopita katika Ligi Kuu ya England ni 38,312 na ndiyo mkubwa zaidi kwa ligi zote za Ulaya.
Ujerumani ambao awali walikuwa vinara, wanashika nafasi ya pili, ukubwa wa viwanja vyake wastani ni 47,775 lakini ule wa watazamaji umeporomoka hadi kufikia 35,852.

Hispania wenye wastani wa 39,612 kwa viwanja, mahudhurio ni chini, kwani wastani ni watazamaji 22,264 na Serie A ndiyo chini zaidi maana wao wana 18,789.

Mabao baada ya dakika 80:
Moja ya vigezo vya ugumu au ubora wa ligi ni mechi kutokuwa na mshindi anayetabirika, baada ya mechi 50, takwimu zinaonyesha mechi za Premiership ndiyo ngumu zaidi.
Kwani hata dakika 10 kabla ya mechi kwisha, bado kila timu inakuwa haijajihakikishia ushindi labda iwe inaongoza kwa mabao 3-0.

Premiership ina asilimia 18.7 za ugumu, kwamba timu zinazopambana zinakuwa imara zaidi na hakuna anayejihakikishia ushindi.

Serie A ni asilimia 17, hii inaonyesha mechi zake nyingi zimekuwa ngumu na zisizotabirika hata baada ya dakika ya 80.
Hispania na La Liga yao ni asilimia 14, wakati Bundesliga imeporomoka kwa kuwa na asilimia 13, maana yake ni timu chache zinazofunga mabao katika dakika 10 za mwisho kwenye ligi hiyo.

Nyumbani & ugenini:
Ligi ya England inazidi kuonyesha ni ngumu na takwimu zake zinaonyesha hivi, hata timu zinapokuwa zinacheza nyumbani, hazina uhakika wa kushinda mechi kuliko ilivyo katika ligi nyingine nyumbani.

Mfano, timu za England zinapocheza nyumbani, zina uhakika wa kushinda kwa asilimia 44 tu, tena kwa wastani wa mabao mawili tu. Kwa Bundesliga wenyewe ni asilimia 55.6 na wengine; (La Liga 46.7% na 46% kwa Serie A).

Mabao:
Kingine ambacho kinaonyesha Premiership ni ligi ngumu ni kutokana na uhaba wa mabao ikionyesha kila timu inakuwa imejizatiti na ina safu ngumu ya ulinzi.
Katika mechi 50 zilizopita kabla ya mechi za juzi Jumamosi, jana Jumapili na leo usiku, mabao yaliyokuwa yamefungwa kwenye Premiership ni 107 tu.

Ukiangalia takwimu za ligi nyingine zinaonyesha mabao yaliyofungwa ni mengi zaidi, mfano mzuri ni Bundesliga, katika mechi 54 zilizopita, mabao 176 tayari yametinga kimiani.

La Liga katika mechi 60, mabao 178 yalikuwa yamegusa nyavu na Serie A, katika mechi 50 nyavu zilikuwa zimetikisika mara 152.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic