Meneja wa Klabu
ya Kagera Sugar, Mohamed Hussein, amesema pamoja na kuwepo kwa malalamiko mengi
juu ya ubovu wa Uwanja wa Kaitaba ambao unatumiwa na timu yao kama uwanja wa
nyumbani, bado na wao ni wageni wa dimba hilo kwani huutumia siku ya mechi tu.
Uwanja huo
unaomilikiwa na Manispaa ya Bukoba, unadaiwa kuwa miongoni mwa viwanja vibovu
Tanzania vitumikavyo kwenye ligi kuu na kudaiwa kuwa chanzo cha matokeo mabaya
kwa timu ngeni.
Akizungumza
na Championi Jumatano, Hussein alisema Kagera Sugar huutumia siku ya mechi tu
kwani kuna uwanja wenye hadhi zaidi ya Kaitaba ambao wanautumia kwenye mazoezi
na maandalizi ya mechi mbalimbali.
“Pale
(Kaitaba) na sisi ni wageni. Tunautumia wakati wa mechi tu, maana maandalizi ya
mchezo wowote huwa tunafanyia kwenye uwanja wetu wa Kagera A, uliopo Misenyi
wakati Kaitaba upo Bukoba,” alisema Hussein.
Aliongeza kuwa,
Kagera A una kiwango kizuri zaidi ya Kaitaba, lakini tatizo lake haujatimiza
masharti ya Fifa, likiwemo la kukosa uzio (fensi) na kusema wameanza mradi wa
kuboresha uwanja wao ili kuachana na Kaitaba msimu ujao.
Tayari kikosi
cha Kagera kimeingia kambini kujiwinda na mchezo wa Jumamosi dhidi ya Yanga
utakaopigwa kwenye uwanja huo wa Kaitaba.
0 COMMENTS:
Post a Comment