Na Saleh
Ally
Mshambuliaji nyota wa Manchester United, Wayne Rooney, anatambuliwa kuwa mmoja wa wanasoka
bora zaidi duniani katika kipindi hiki.
Rooney
ambaye alichipukia Everton jijini Liverpool, amekuwa gumzo tangu akiwa na umri
wa miaka 16, akiwa na Everton mwaka 2002, alifunga bonge la bao dhidi ya
Arsenal, dunia ya wanamichezo ikaanza kumzungumzia.
Baada ya
hapo, Manchester United ilishindwa kujizuia, Kocha Alex Ferguson akaushawishi
uongozi kutoa kitita kikubwa cha pauni milioni 30 kwa mchezaji kinda kama yeye,
akasisitiza kwamba hawatajuta kutoa dau hilo, kweli ndivyo ilivyokuwa.
Achana na alivyoanza hadi kufikia alipo,
lakini moja ya upungufu mkubwa alionao Rooney, hasa uwanjani ni kushindwa
kudhibiti hasira zake, mara nyingi zimemzidi nguvu na kufikia kufanya uamuzi
ambao alijilaumu.
Amewahi
kupata kadi nyekundu mara kadhaa kutokana na utukutu wake, aligombana mara kadhaa
na aliyekuwa kocha wake, Alex Ferguson na ikafikia hadi kuamua kuandika barua
kwamba anataka kuondoka Manchester United.
Vurugu hizo
zilisababisha mashabiki wa Manchester United washindwe kujizuia na kumzomea
siku alipokabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu England na kuliinua juu.
Binadamu
wanabadilika, takwimu zinazidi kuonyesha Rooney ni kati ya wachezaji bora
duniani lakini hasira zake ambazo ni sawa na shetani kwake, sasa amezishinda.
Sakata la
kutoelewana na Ferguson hadi ujio wa David Moyes, bado ameendelea kuwa kimya.
Wakati wengi wakiendelea kumjadili na mambo mengi yakizagaa, Rooney baba wa
watoto wawili, ameonyesha yuko tofauti.
Hakubishana
au kupingana na kocha, mchezaji, shabiki wala vyombo vya habari. Badala yake
akaendelea kupiga kazi kama kawaida.
Kazi yake
ndiyo imewanyamazisha wengi, amecheza mechi sita akafunga mabao matatu huku
akiwa na pasi mbili zilizozaa mabao mawili.
Katika
mechi hizo sita za msimu wa 2013, Rooney amepiga mashuti 18 yaliyolenga lango na
kuwa mmoja wa wachezaji wachache waliofanya hivyo katika Ligi Kuu England.
Kelele
zilipungua, lawama zikaanza kuzimika, shangwe zikaongezeka, pongezi zikachanua
na hakuna anayesema vibaya tena kuhusu yeye.
Kayamaliza
matatizo kiutu-uzima, ameonyesha kazi ni kiboko ya maneno mengi. Huenda hili ni
funzo kwa wengine na wanaweza wakautumia mfumo wake huo wa kumshinda shetani na
kutoa majibu kwa kuchapa kazi.
Takwimu za Rooney Premiership…
MECHI MABAO
PASI MASHUTI
6
3 2 18
0 COMMENTS:
Post a Comment