Azam FC imepaa hadi kileleni kwa
kufikisha pointi 23 baada ya kufanikiwa kuwashusha kileleni Simba kwa kuwachapa
kwa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara,
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kufunga katika dakika ya 21 kupitia kwa
Ramadhani Singano ambaye aliupachika mpira kimiani kwa ufundi mkubwa.
Lakini dakika moja kabla ya kwenda
mapumziko, Kipre Herman Tchetche akafunga bao la kusawazisha baada ya
kuunganisha vizuri krosi safi ya Erasto Nyoni.
Kipindi cha pili, kila timu ilishambulia
kwa kasi huku ikionyesha kila upande ulitaka kupata bao la pili.
Lakini Azam FC ndiyo walifanikiwa kupata
bao zikiwa zimebakia dakika 13 tu mpira kwisha baada ya Tchetche tena raia wa
Ivory Coast kufunga kwa ustadi mkubwa baada ya kumkalisha kipa Abel Dhaira.
Simba ilijitahidi kupata bao la pili,
lakini mambo yalionekana kuwa magumu na nusura Azam FC wapate bao la tatu baada
ya Tchetche aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita kuingia katika eneo la
hatari na kufumua shuti kali, lakini Dhaira akafanya kazi ya ziada.
0 COMMENTS:
Post a Comment