Mapenzi ni kitu muhimu sana katika muongozo
wa mambo mengi, iwe katika michezo au maisha ya kawaida.
Kunapokuwa na upendo mambo mengi yanaweza
kwenda kwa uhakika, ukipotea, amani inatoweka na kila kitu kinayumba na mara
nyingi haki inapotea.
Mchezaji nyota wa kikapu wa mabingwa wa Ligi
ya Kikapu ya Marekani (NBA), Miami Heat, Dwyane Wade, amesisitiza kuwa upendo
ndiyo nguzo ya kila kitu anachofanya na kufanikiwa zaidi, anatamani kuona
anayempenda zaidi ana furaha.
Wade ambaye sasa ni mmoja wa wanamichezo
wanaolipwa fedha nyingi duniani, ameamua kuwa mfano, kamnunulia mama yake mzazi,
aitwaye Jolinda, kanisa kwa kutoa dola milioni 2 (zaidi ya Sh bilioni 3.2).
Wade kamwaga fedha hizo kwa mama yake ambaye
alishindwa kumlea mwanaye kutokana na kuwa ‘teja’, mtumia madawa ya kulevya
hadi akakumbana na kifungo gerezani.
Sasa Jolinda ni mchungaji na kanisa lake
lina umaarufu mkubwa, lakini kabla ya hapo miaka nane alikuwa jela baada ya
kupatikana na hatia ya kuuza na kutumia madawa ya kulevya.
Alishindwa kumlea mwanaye na hata wakati
anaanza kupata mafanikio, hakuwa akijua lolote. Badala yake alimshuhudia tayari
amefanikiwa na wengi wakaamini Wade angekuwa na kinyongo na mama yake.
Maisha yake yote, Wade alikosa mapenzi ya
mama kwa kuwa alilelewa na dada yake mkubwa aitwaye Tragil. Mama yake alionekana amepotea, ndugu
walijaribu kumbadilisha bila ya mafanikio. Jumapili moja, mwaka 2001, Tragil alifanikiwa kumshawishi mama yake ahudhurie kanisani,
mabadiliko yakaanzia hapo.
Baada ya siku ya kwanza
kanisani, Jolinda alikubali kuanza tiba ya kuondoa madawa ya kulevya mwilini
mwake katika Mji wa Illinois.
Baadaye Jolinda alikubali kuingia katika
maombi na mwisho akakubali kushiriki mambo mbalimbali ya kanisani.
Oktoba 2007, Jolinda akachukua
uamuzi wa kupangisha chumba kwa ajili ya kuanzisha kanisa na alifanikiwa kupata
watu 47 waliokuwa wakisali katika kanisa lake, yeye akijulikana kama Mchungaji
Jolinda.
Baada ya kutoka jela, pamoja na kwamba hakuwahi kuonyesha mapenzi kwa
mwanaye, Wade hakuwahi kupunguza mapenzi kwa mama yake, kwani alimnunulia gari na
nyumba.
Aliposikia ameamua kuanzisha kanisa, siku moja alihudhuria kanisani
kwake na kumkuta akihubiri katika chumba kidogo tu. Ndipo alipochukua uamuzi
huo wa kutoa dola milioni moja na kununua jumba kubwa kwa ajili ya kanisa la
mama yake.
Jumapili, Mei 18, Jolinda Wade alifungua kanisa lake na katika
uzinduzi pamoja na Wade, nyota kadhaa kama Shaquille O’Neal na Magic Johnson,
walihudhuria.
Simulizi kuhusu ilivyokuwa, inaweza kuwa ndefu sana. Lakini alichosema
Wade ni kwamba miaka yote alikuwa na ndoto ya kufanya vizuri ili amsaidie mama
yake ambaye amekuwa akishukuru sana kwa angalau kidogo anachompa.
Kumbe inawezekana kumtumia mzazi kama changamoto, yaani ukiona una
majukumu na unataka kumfurahisha, basi ni rahisi kufanikiwa kwa kuwa kila
kukicha utaongeza juhudi.
Wanamichezo wengi nchini wana uwezo mkubwa, lakini hawana juhudi wala
ndoto ya kufika mbali kwa kuwa huenda hawafikirii kwamba wana jukumu la kuwapa
furaha wazazi wao kama wakifanikiwa.
Wade kafanikiwa zaidi kupitia kuwa na ndoto ya kutaka kumsaidia mama
yake. Hata nyumbani hapa inawezekana.
Vidokezo:
*Mwaka 1994, Jolinda alikamatwa kwa kukutwa akiuza madawa ya kulevya.
Wade akaenda kumtembelea jela, yeye akamuomba Mungu amsaidie kumlinda mwanaye.
*Mwaka 1998, Jolinda alitoka jela kupitia utaratibu maalum wa kufanya
kazi unaosimamiwa na magereza, baadaye akarudishwa tena jela.
*Mwaka 1998, Jolinda akatangaza kuachana na pombe na kuvuta sigara.
Akapokea barua ya kumpa moyo kutoka kwa Wade aliyemueleza mama yake kwamba
ndiye shujaa wake. Akiwa gerezani, akaamua kuokoka.
Mwaka 2003, Jolinda akamaliza kifungo na kwa mara ya kwanza akaenda
uwanjani kumuona mwanaye akicheza mechi ya mpira wa kikapu.
Baada ya mechi alitangaza kushangazwa na alichokifanya mwanaye
uwanjani, hakuwahi kumuona kabla. Akasisitiza kutogusa tena madawa kwa kuwa
ametubu na asingependa kumsumbua mwanaye tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment