October 7, 2013




Na Saleh Ally
Uimara wa timu zinazoshiriki ligi husika ndiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka umaarufu wa ligi.

Ligi Kuu ya England maarufu kama Premiership ndiyo ligi ya soka maarufu kuliko zote duniani na hali hiyo huenda ikapanda zaidi kutokana na ugumu unavyozidi kupanda.


Inaonekana kumekuwa na mabadiliko makubwa katika hatua za mwanzo huku timu kubwa kama mabingwa Manchester United, zikipata wakati mgumu kutoka kwa timu nyingine ambazo zilikuwa hazipewi nafasi.

Ugumu unaongeza umaarufu lakini unachangia watu wengi kutamani kwenda kuzishuhudia mechi uwanjani badala ya kubaki nyumbani au kwenye baa na kuangalia katika runinga.

Ikiwa bado ligi mbichi kabisa, bila ya kujumuisha mechi zilizochezwa jana Jumapili, mashabiki 2,399,903 walikuwa wameingia uwanjani kushuhudia michezo mbalimbali ya ligi hiyo.

Idadi zaidi ya watu milioni katika kipindi hicho kifupi, maana yake ni dalili ya kukubalika zaidi kwa kuwa haijafikiwa na ligi nyingine.

Kama hiyo haitoshi, inaonyesha timu za England zitaendelea kupata faida kubwa kupitia katika nyanja mbili zinazotegemewa katika uingizaji wa mapato.

Kwanza ni viingilio vya uwanjani kwa kuwa mashabiki wanamiminika kwa wingi, pili ni wadhamini kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa kuwa wataamini kuingia mikataba na timu za Premiership ni nafasi nzuri ya kutangaza bidhaa zao.
Mfano mzuri kwamba ligi hiyo sasa inakubalika zaidi ni ile mechi iliyoingiza watu wachache zaidi, iliwakutanisha Swansea City walipokuwa nyumbani dhidi ya Arsenal na watu uwanjani walikuwa 20,712.


Mechi iliyoingiza watu wengi zaidi ni ile iliyopigwa juzi kati ya wenyeji Manchester United dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Old Trafford. Watu 75,170 wakajitupia uwanjani.

Hapa kuna kitu cha kujifunza, kwamba pamoja na ubora wa ligi, lakini mazingira ya viwanja husika yanachangia watu hata kuona wako salama, hakuna bughudha na ni salama.

Maana yake wana uwezo wa kuchukua hadi familia zao, mfano mke na mtoto na kwenda nao uwanjani, vitu ambavyo ni vidogo na vinapaswa kutupiwa macho hata hapa nyumbani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic