Na Richard Bukos, Tanga
KOCHA Msaidizi wa Simba,
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, juzi Jumatano alikuwa katika wakati mgumu na
kulazimika kuzichapa na shabiki ambaye alimvaa na kumtupia maneno makali.
Mashabiki akadhaa walimtuhumu
kuchukua mlungula na kusababisha timu hiyo kushindwa kufanya vizuri baada ya kuambulia
suluhu katika mechi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Baada ya mechi hiyo mashabiki
hao walimfuata Julio nyuma ya jukwaa kubwa na kumzonga huku wakimtupia lawama
kwa kuihujumu timu yao.
Julio alipoona mashabiki
hao wanaendelea kumtolea lugha kali, naye alikazana kuwajibu kwa kuwatolea
lugha kali, baada ya mabishano kushika kasi, Julio akitumia makabrasha
aliyokuwa ameyashika, akaanza kumpiga nayo shabiki mmoja kichwani.
Baada ya kuona vuta nikuvute
imezidi ndipo askari wa kutuliza ghasia waliitwa kutuliza zogo hilo ili kocha
huyo aondoke kwa amani uwanjani hapo.
“Wewe tushakujua mtu wa ‘ten
percent’, huna lolote, unaacha kuchezesha wachezaji wa maana unatuwekea
makanyanga yako,” alisikika shabiki huyo aliyetwangwa na makabrasha kichwani.
“Kwani we nani kwenye
timu hii, umeshawahi kuisaidia nini Simba kwenye maisha yako? Hata kadi huna hapo
ulipo,” alisikika Julio akijibu mashambulizi huku akiingia kwenye gari aina ya
Mitsubishi Erandis yenye namba za usajili T 404 CBJ.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment