Kocha Mkuu wa Kenya, Adel Amrouche,
amechukizwa na kufutwa kwa mchezo wa timu yake dhidi ya Taifa Stars, lakini
akawaomba radhi wananchi wote wa Tanzania.
Stars ilipaswa kucheza na Kenya, kesho
Jumanne kwenye mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini
mtanange huo umeahirishwa kutokana na matatizo ya mawasiliano, hivyo Stars
itakipiga na Zimbabwe kesho kwenye uwanja huo.
Amrouche raia wa Ubelgiji, amesema taarifa za kufutwa
kwa mchezo huo zimemkosesha raha, kwani alitarajia Stars ingekuwa kipimo kizuri
kwa kikosi chake.
Amrouche aliyewahi kuifundisha Burundi
kabla ya Kenya, amesema kikubwa kilichosababisha mechi hiyo kufutwa ni tatizo
la mawasiliano kati ya Chama cha Soka cha Kenya (KFF) na nyota aliowataka kujiunga
na timu hiyo.
“Nawaomba radhi Watanzania wote, sikutarajia
kama hilo lingeibuka, nilitarajia kupata upinzani mzuri kutoka kwa Tanzania,
kitu ambacho sasa kimekosekana,” alisema Amrouche na kuongeza:
“Kuna moja ambalo limesababisha
kuahirishwa kwa mechi hiyo, chama cha soka huku hakikuwa na mawasiliano mazuri
na klabu ambazo wachezaji wake niliwachagua, kitu ambacho kilisababisha hata
kambi yetu kuchelewa.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana na
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kiingilio cha chini cha
mchezo huo wa kesho ni Sh 5,000.
“Mbali ya kiingilio hicho cha Sh 5,000
ambacho ni kwa viti vya bluu na kijani, viingilio vingine ni Sh 30,000 kwa VIP
A, Sh 20,000 kwa VIP B, Sh 15,000 kwa VIP C, wakati viti vya rangi ya chungwa
ni Sh 10,000,” alisema Wambura.
0 COMMENTS:
Post a Comment