Hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara
unamalizika, tumeona namna kikosi cha Mbeya City chini ya Kocha Juma Mwambusi
ambavyo kimekuwa gumzo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka.
Achana na kwamba Mbeya City imemaliza
mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi ya tatu juu ya timu kama Simba, lakini
bado ilionyesha soka safi na la kuvutia kwa kila timu iliyokutana nayo.
Angalia kwa timu kongwe kama Yanga,
Simba na Azam FC ambayo imekuwa ni moja ya timu ngumu, kati ya hizo hakuna
ambayo imeifunga Mbeya City, kila moja imeambulia sare na ukiangalia sare mbili
timu hiyo imepata ikiwa ugenini dhidi ya Simba na Azam FC.
Ligi imefikia tamati katika mzunguko wa
kwanza na imeacha mambo mengi sana ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kama somo
na si kuachwa yapite.
Mbeya City hadi ilipofikia haikuwa ni
kitu cha kukaa na kuota tu, badala yake walifanya kazi. Kwao ni watu
wanaotakiwa kutobweteka na kufikiri mambo yalienda kwa kuhatisha tu au
walipofikia ndiyo mwisho, ligi haijaisha.
Kwa timu nyingine, zikiwemo zilizo
katika nafasi za chini lazima ziamini kuwa mzunguko wa kwanza umekuwa na
changamoto, hivyo somo ni kuangalia wapi waliteleza na nini cha kufanya kwa
kipindi hiki cha mapumziko ya ligi.
Simba na Yanga pia, ni timu kongwe
lakini imeonekana wazi kwamba mzunguko wa kwanza umekuwa mgumu kwao na ukongwe
wao haukuonekana kama inavyotakiwa.
Angala Yanga ilianza ligi kwa kusua,
ikaenda inabadilisha gia hadi kufikia ilipokuwa na imemaliza inaongoza. Lakini
Simba ilianza vizuri na mwisho ikaenda inaporomoka kila kukicha na imeishia
katika nafasi ya nne.
Huu ni wakati wa mapumziko, lakini
hakuna mtu makini awe mchezaji, kocha au kiongozi anaweza kupumzika na kulala
eti kwa kuwa ndiyo kipindi cha kupumzika kimefika. Inawezekana kupumzika lakini
kazi nzuri hufanywa katika kipindi cha utulivu.
Ninamaanisha hivi, kila mmoja kwenye
upande wake anapaswa kujitathmini, kwamba alichezaje, alifundishaje,
aliongozaje na baada ya hapo ni nini cha kufanya.
Wachezaji wanapaswa kufanya mazoezi ya
ziada ili kukabiliana na mzunguko wa pili wa lala salama ambao huwa mgumu zaidi
kwa kuwa ni sawa na mtihani shule, kwamba itajulikana umepata daraja lipi.
Kwa makocha, huu si wakati wa soka tu,
wasome, waangalie walichofanya na nini cha kuongeza. Maneno mengi halafu uwezo
wa kazi hakuna pia si kitu kizuri. Kwa upande wa viongozi pia nao wanapaswa
kuangalia waliposhindwa kuziongoza vizuri timu zao.
Vizuri itakuwa kiwango kilichoonyeshwa
mzunguko wa kwanza, kipande zaidi katika mzunguko wa pili na hakiwezi kupanda
kama sikukuu itakuwa ndefu na wachezaji, makocha na viongozi watalala hadi kusubiri siku chache kabla ya
ligi kuanza, eti ndiyo waanze kujiandaa.
Ndoto ya mafanikio katika kitu chochote
ndiyo jambo la kwanza la msingi, kwamba nataka kufanya hivi, kufikia hapa.
Lakini siku zote hicho hakiwezi kufanikiwa kama ufanisi ni ziro.
Ndani ya ufanisi kuna juhudi na maarifa,
kama hauna maarifa umekwama lakini haujitumi, mwisho utaishia kusema umepigwa
misumari na huo utakuwa mwisho wako.
0 COMMENTS:
Post a Comment