Na Waandishi Wetu, Shinyanga na Moshi
Mashabiki
wa Simba wameendelea kutangaza ubabe kwa mashabiki wa Yanga baada ya kuwashinda
kwenye mechi za mashabiki hao zilizochezwa jana kwenye miji ya Shinyanga na
Moshi kupitia bonanza la Nani Mtani Jembe, lililoandaliwa na Kilimanjaro
Premium Lager ambapo pote Simba walishinda.
Hata hivyo Yanga waliweza kujipoza
huko Moshi kwa kupata ushindi mnono kwenye michezo ya kufukuza kuku, kupiga
penati kwenye goli dogo na kupiga danadana.
Shinyanga
bonanza lilianza mwendo wa saa 9 alasiri ukitangulia mchezo wa kufukuza kuku
ulitangulia ambapo mashabiki wa Simba waliibuka washindi dhidi ya Yanga. Baada
ya hapo ulifuata mchezo wa kukimbia ukiwa umevaa gunia ambapo Charles Shija wa
Simba aliibuka kinara kwa mikimbio 2 dhidi ya 1 wa Yanga.
Ulifuata mchezo wa
kuvuta kamba wanaume ambapo pia Simba walishinda yanga 2-1.
Baada
ya mchezo huo kulifuata mechi kali sana kati ya mashabiki wa Simba wa soka wa
mkoa wa Shinyanga na mashabiki wa soka wa Yanga, ambapo katika mechi hiyo simba
walipata penati kipindi cha kwanza na mchezaji Iddi Mobi hakufanya ajizi na
kukwamisha mpira wavuni. Mpaka mapumziko Simba 1 Yanga 0.
Kipindi cha pili
Yanga walikuja juu ili wasawazishe lakini bahati haikuwa kwao na kujikuta
wanapachikwa bao la pili lililofungwa na Kulwa Mobi. Baada ya bao hilo Yanga
walikuja juu na dakika 8 kabla ya kipenga cha mwisho walipata penati iliyotiwa
nyavuni na Amani Rashid. hivyo mpaka filimbi ya mwisho Simba 2, Yanga 1.
Huko
Moshi mashabiki wa Yanga walishinda mchezo wa kupiga dana dana na kupiga penati
kwenye goli dogo, kufukuza kuku. Kwenye mchezo wa soka, mashabiki wa Simba
walishinda kwa goli 2 – 1 na pia walishinda kuvuta kamba. Bonanza hilo
lilipambwa na Malindi Band, Msanii maarufu wa bongo flava wa Moshi
ajulikanae kama Majirani pamoja na wasanii wa kundi la Black Warriors.
Kupitia
kampeni ya Nani Mtani Jembe, bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini
timu za Simba ya Yanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 na kisha
kuzigawanya kwa timu hizo ambapo kila timu inazo shilingi milioni 50 ambazo
zinashindaniwa na mashabiki wao.
Meneja
wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema kuwa mashabikiwa Simba na Yanga
wanatakiwa kushindana kwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ili kuhakikisha kuwa
timu mojawapo inapata fedha nyingi zaidi ya timu nyingine.
Akielezea
namna ya kushiriki, Kavishe alisema kuwa mpaka kila timu imetengewa shilingi
milioni 50 na kuwa mshiriki wa shindano hilo la Nani Mtani Jembe ambaye ni
shabiki wa Simba au Yanga anachotakiwa kufanya ni kununua bia ya Kilimanjaro
ambayo kwenye kizibo chake kuna namba ya kushiriki.
Alisema
baada ya shabiki kununua bia ya Kilimanjaro na kuona namba ya kwenye kizibo,
anachotakiwa kufanya ni kuchukua simu yake ya kiganjani na kuandika ujumbe
mfupi wa maneno akianza na jina la timu anayoshabikia kisha anaandika namba
iliyo kwenye kizibo na kuituma kwenye namba 15440.
Alisema
baada ya shabiki kutuma namba hiyo, atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka
kwa timu pinzani yaani ikiwa shabiki aliyetuma ujumbe huo ni wa Simba atakuwa
amefanikiwa kupunguza shilingi 10,000 kutoka kwenye fungu la Yanga na ikiwa
shabiki ni wa Yanga pia atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka kwa Simba.
Kwa
mujibu wa Kavishe matokeo ya uwiano wa fedha zinavyopungua kutoka Simba au
Yanga yatangazwa kila siku hadi siku ya mwisho wa shindano hilo Desemba 14,
mwaka huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment