Na Saleh Ally
Nusu msimu baada ya kumuacha Juma
Kaseja ikidai ameshuka kiwango, Simba imekuwa na matatizo makubwa katika nafasi
ya kipa.
Lawama kwamba Kaseja alikuwa anaachwa
kutokana na masuala ya siasa za soka na wala si uwezo zilipingwa vikali na
viongozi hasa wale wa kamati ya usajili ya Simba.
Sasa hakuna ubishi tena kwamba siasa
zimewaumbua Simba, kwamba Kaseja hakuwa ameshuka kiwango na badala yake kipa
Mganda Abel Dhaira aliyekuwa anawekewa nafasi ya kucheza ndiyo hakuwa na
kiwango kizuri.
Tayari Simba iko katika hatua za
mwisho za kuachana na Dhaira na haina ujanja wa kumpata Kaseja na badala yake
imelazimika kumsajili kipa Yaw Berko aliyewahi kudakia Yanga.
Berko raia wa Ghana aliletwa nchini
na Kocha Mserbia, Kosta Papic ambaye aliwahi kufanya naye kazi nchini humo
kabla ya kutua nchini na kuifundisha Yanga.
Berko anakuja nchini kuifanyia Simba
kazi kwa nusu msimu na baada ya hapo hatakuwa na ujanja maana atalazimika
kuondoka nchini baada ya kuanza kwa kanuni mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), timu kutosajili makipa wa kigeni.
Berko si mgeni katika soka nchini,
anajulikana kwa mambo kadhaa lakini matatu yanaweza kuwa maarufu zaidi
kuhusiana naye.
Kwanza ni mpole na anayetumia muda
wake mwingi kusajili, muoga wa ushirikina, mwenye tabia ya kususa lakini
anajulikana kuwa ni kipa mwenye uwezo wa juu na Simba inaweza kufaidika na yale
ambayo ni mazuri.
Kusali:
Ni nadra kumuona Berko akiwa hana
rozali shingoni mwake, mara nyingi amekuwa akitumia muda mwingi akiwa na Biblia.
Muumini huyo Mkristo ni mtaratibu na
mara nyingi hupenda kuwa peke yake, katika mahojiano yake huko nyuma na gazeti
hili amewahi kusema hawezi kuanza mazoezi au kucheza mechi bila ya kumuomba
Mungu na kila anapomaliza lazima afanye hivyo.
Ushirikina:
Pamoja na kuwa mcha Mungu kwa sana,
Berko amekuwa na sifa ya kuhofia ushirikina kupita kiasi, huenda ni kutokana na
nchi ya Afrika Magharibi anayotokea.
Aliwahi kulalamika hadharani kuwa
kipa mwenzake wakati huo, Shabani Kado alikuwa anamfanyia vitendo vya
kishirikina ndiyo maana akawa anashindwa kudaka vizuri.
Kutokana na hali hiyo ukazuka
mtafaruku kati ya Berko na Kado lakini uongozi wa Yanga ukaingilia na kulifukia
suala hilo lakini siku chache baadaye Kado aliachwa na Mghana huyo akaendelea
kubaki Yanga.
Kususa:
Suala la kususa limekuwa ugonjwa wake
mkuu, lakini hadi anaondoka Yanga alishika nafasi ya kuwa kipa ‘anayedeka’
kuliko wote katika timu 14 zinazoshiriki ligi kuu.
Mfano amekuwa mgonjwa wa bega, lakini
anapoona mashambulizi makali yanaelekezwa langoni mwake,ni rahisi sana kusema
anasikia maumivu na kutoka.
Hali hiyo ilikuwa inamuudhi sana
Papic na aliwahi kuizungumzia lakini mara ilipoonyesha kumuudhi Ernie Brandts
baada ya Berko kusema bega linamuuma anataka kutoka, basi hakumrudisha tena na
moja kwa moja akaamua kumpa nafasi ya kipa wa kwanza Ally Mustapha ‘Barthez’.
Baada ya hapo ndiyo safari ya Berko
kurejea Ghana ikamkuta kwa kuwa ilionekana Brandts ameamua kumtumia Mtanzania
huyo aliyetokea Simba kama kipa namba mbili.
Uwezo:
Hakuna ubishi kila mtu ana uwezo wa
kuchagua lakini namba ya Berko kwa makipa katika ligi kuu ni moja au mbili na
mshindani wake mkubwa anaweza kuwa Kaseja.
Berko ana uwezo wa juu kabisa na
alionyesha hilo akiwa Yanga hata pale safu ya ulinzi ilipoonekana kupoteza
uelekeo.
Berko ni mzuri kudaka mipira ya krosi
inayoelekezwa langoni mwake lakini ana kasi zaidi katika kupangua mipira ya
pembeni.
Burudani zaidi kutoka kwa Berko ni
‘timing’ ya kuziba lango hasa anapokuwa amebaki na mshambuliaji mmoja ambaye
anajaribu kufunga.
Pamoja na hapo, kipa huyo hauwezi
kumuondoa katika tatu bora ya makipa wenye uwezo mkubwa wa kudaka mikwaju ya
penalti na alilionyesha hilo Yanga ilipocheza na Simba katika fainali ya Ngao
ya Jamii, mwaka juzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment