Mlezi wa Simba, Rahma Al Kharusi
amefunguka na kusema ndani ya klabu hiyo kumekuwa na matatizo mengi kwa kipindi
kirefu.
Rahma maarufu kama Malkia wa nyuki,
amesema Simba ina nafasi kubwa ya kuendelea lakini kutoelewana kati ya
Mwenyekiti, Ismail Aden Rage na viongozi wenzake kumekuwa ni tatizo kubwa na
pande zote mbili zinasababisha mgawanyiko.
Akizungumza katika mahojiano maalum
jana, Malkia wa nyuki amesema kila upande unaweza kuwa na sehemu ya kuchota
lawama ingawa sasa si kipindi mwafaka cha kufanya hivyo.
“Kama nilivyosema awali, mimi sina
upande ndani ya Simba, siko kwa Rage wala kamati ya utendaji. Upande wowote
naweza kushirikiana nao kama unalenda kuleta maendeleo kwenye klabu.
“Lakini kila upande, ninamaanisha
mwenyekiti (Rage) hata baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji nao ni matatizo
na si ya leo tu, yamekuwa yakikua taratibu hadi leo yamefikia hapa.
“ Kuna mambo mengi yanaonyesha ubinafsi wao,
wengine wanahofia wengine kupata sifa, vizuri kama wangetanguliza maendeleo ya
klabu kwanza, sifa baadae.
“Wako watu wanafanya kazi kwenye klabu
kwa ajili ya maslahi yao binafsi, hawataki kuona mambo yanakwenda haraka na
hasa kama wakiona hawafaidiki.
“Mimi ni msemakweli na wala sina hofu.
Kikubwa hapa ni kumaliza matatizo ya sasa ili tuendelee mbele kwa ajili ya
kuwatumikia Wanasimba na kuleta maendeleo.
“Inawezekana kuleta maendeleo, lakini kama watu
watakuwa wabinafsi basi hakutakuwa na maendeleo yatakayopatikana. Sitaki kusema
mambo mengi sana zaidi ya hapa,” alisema Malkia wa nyuki.
Malkia wa nyuki sasa ni mmoja wa wajumbe
wa bodi ya wadhamini wa Simba, cheo ambacho amepewa na Rage aliyekuwa tayari
ametangazwa kusimamishwa lakini mwenyewe akapinga kuhusiana na hilo na kusema
walikiuka katiba.
Lakini baadhi ya wachambuzi wa mambo
wanaeleza kuwa Rage ameamua kumuondoa ndani ya kamati ya utendaji ili apate
nafasi nzuri ya kupambana na waliobaki.
0 COMMENTS:
Post a Comment