LUIZIO KAZINI |
Na Saleh Ally
Tayari taarifa za timu fulani kumtaka huyo na nyingine kumtaka yule, zimeanza kwa kasi
katika vyombo mbalimbali vya habari.
Inajulikana
wazi timu mbili za Simba na Azam FC zimekuwa zikihaha kupata makocha, hata kama
viongozi watakataa kama ilivyo kawaida ya wengi, lakini ukweli ni kwamba
zinaendelea kufanya mazungumzo na makocha kadhaa.
Pamoja na
kuendelea kufanya mazungumzo na makocha kadhaa, suala la kutaka kusajili
wachezaji halijasimama na wale wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara watakuwa
ni kati ya wanaowindwa sana.
Washambuliaji
wameendelea kuwa tatizo kwa Tanzania, hasa kwa wazawa. Lakini safari hii
imeonekana hivi, wazawa wa Yanga, Azam FC na Simba wamekuwa hawana kasi kubwa
sana ya upachikaji mabao kama ilivyo kwa wageni.
Wageni kutoka
timu hizo tatu ndiyo wanaonekana kuwa na uwezo wa juu zaidi huku wakishindana
na wazawa walio katika timu nyingine kama Mbeya City, Ruvu Shooting na Kagera
Sugar.
Mrundi wa
Simba, Amissi Tambwe ndiye anaongoza kwa upachikaji mabao, sasa ana mabao 10
akiwa kileleni na anafuatiwa na Elius Maguri wa Ruvu Shooting akiwa mzawa wa
kwanza msimu huu kufikisha mabao tisa.
Halafu Mganda
wa Yanga, Hamis Kiiza mwenye nane, sawa na mzawa mwingine, Juma Luizio wa
Mtibwa Sugar na chini ya hapo unamkuta Kipre Herman Tchetche, raia wa Ivory
Coast mwenye mabao saba.
Mabao sita
kushuka chini, utawakuta wazawa wakiwa kwa wingi wakipambana na wageni wachache
kama Didier Kavumbagu wa Yanga kutoka Burundi mwenye mabao matano na Mkenya,
Jerry Santo wa Coastal Union mwenye manne.
Wazawa
wengine ambao wanaonyesha kasi kidogo ni Mrisho Ngassa (Yanga) na Themi Felix
(Kagera Sugar), kila mmoja akiwa ana mabao sita.
Hii ni dalili
kwamba timu zenye nguvu ya fedha lazima zitaelekeza nguvu zao kwa wachezaji
wazawa wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ambao katika mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu Bara wameonyesha wanaweza.
Hakuna ubishi
Maguri wa Ruvu Shooting atakuwa anayeonekana zaidi na hakuna ubishi huenda kuna
timu zimeanza naye mazungumzo tayari. Mwingine ni Luizio wa Mtibwa Sugar,
mwenye mabao nane na ukiangalia wazawa hawa ndiyo waliowapiku washambuliaji wa
kigeni waliosajiliwa kwa mamilioni ya fedha pamoja na wazawa wenye majina
makubwa.
Lakini kasi
ya wengine wawili ambao ni Felix wa Kagera Sugar na Mwagane Yeya wa Mbeya City
siyo ya kitoto. Hao ni kati ya washambuliaji wanaozungumzwa hivi sasa. Mvuto
wao ni kupachika mabao, kitu ambacho kitatakiwa na timu yoyote ile.
Kila mchezaji
anafanya juhudi ili kufanikiwa zaidi na maana yake sahihi ni kupata maslahi
zaidi. Ni kwamba, kama itatokea mmoja au wawili kusikia wanatakiwa na Yanga,
Simba au Azam FC, basi hawatasita kukimbilia mara moja hilo dau, ndiyo maisha,
wafanye nini!
Pamoja na
hivyo, labda Felix ambaye ni mkongwe sasa hivi, lakini wale ambao ndiyo msimu
wa kwanza wanaonyesha cheche zao, vizuri pia wakajifanyia tathmini na kuangalia
kama wanapaswa kujiunga na timu hizo. Kwamba sasa ni wakati mwafaka?
Kwa kuwa
wanaweza kukimbilia fedha halafu ukawa ndiyo mwisho wao, maana kuna mifano
kadhaa mmekuwa mkiiona.
Angalia
wakati ule Shija Mkina na Simba, alikuwa tegemeo Kagera Sugar lakini Simba
ikaonekana kama alikuwa hana msaada. Mfano mwingine mzuri wa hivi karibuni ni
Hussein Javu ambaye alitokea Mtibwa Sugar na kujiunga na Yanga.
Alikuwa
tishio na hata Yanga walikuwa wanamhofia, wakafanya juhudi kubwa na siku chache
baadaye wakafanikiwa kumpata. Lakini sasa hata benchi tu imekuwa ni bahati
kwake kupata nafasi ya kukaa pale.
Sasa jiulize
kutokea tegemeo katika timu kama Mtibwa Sugar hadi kukosa hata nafasi angalau
ya kukaa benchi tu Yanga. Hii si sawa kwa mchezaji anayetaka kuendelea.
Hapa kuna
mawili, huenda uongozi ulikurupuka na kumsajili kupitia kamati yake ya usajili
bila ya mapendekezo ya benchi la ufundi lakini pili, mchezaji mwenyewe hakupima
kwamba wapi pa kwenda na kama ni Yanga, ilikuwa ni wakati mwafaka?
Usajili wa
mikataba unaanza kabla ya dirisha dogo halijafunguliwa, sasa ni wakati mwafaka
kwa wachezaji kupima mambo kwamba walipo au wanapotaka kwenda kwa kipindi
husika ni wapi sahihi? “Akili mkichwa”.
0 COMMENTS:
Post a Comment