Pamba ya
Mwanza, RTC Shinyanga, Ushirika Moshi, RTC Kigoma, Lipuli Iringa, Majimaji
Songea na timu nyingine kibao ambazo zimebaki majina, leo zinaenziwa na Mbeya
City.
Vuta
subira, twende taratibu nikueleze. Wakati huo nakumbuka nikiwa shule ya msingi,
timu zilizokuwa zinafanya vizuri ukiacha Simba na Yanga, zilikuwa ni zile zilizokuwa
chini ya mashirika mbalimbali kama RTC na mengine.
Wachezaji
wake walikuwa bora, walikuwa tayari kupambana kwa kila namna kuhakikisha timu
zao zinatamba kwa kuwa walikuwa na uhakika wa ajira zao, maana yake uendeshaji
wa maisha haukuwa wa kusuasua tena.
Hili
unaweza kuliona si muhimu sana, lakini wakati ule timu kama Mwadui Shinyanga
ilikuwa inamiliki ndege yake, hakuna anayesema.
Pamba ya
Mwanza ndiyo ilikuwa inaongoza kwa kukodi ndege, mfano ilikwenda Songea, ikatua
mchana, moja kwa moja ikaenda uwanjani na kuiadhibu Majimaji na baada ya hapo ikarudi
kwenye ndege na kupaa kurejea Mwanza.
Leo
ukisikia timu imepanda ndege, basi ni kati ya hizi, Yanga, Simba au matajiri
Azam FC. Timu nyingine hata safari za kawaida kwenda kwenye vituo vya ligi,
imekuwa tatizo kubwa.
Simba na
Yanga zina uhakika kwa kuwa nazo zimepewa mabasi na wadhamini, lakini kabla ya
hapo, usafiri wao ulikuwa ni wa kuungaunga tu, oh! Hapa nilikuwa nakumbushia
tu.
Maana hata
baada ya mashirika kuachana na timu hizo, zilitua mikononi mwa wananchi na
zikaendelea kufanya vizuri, nakumbuka RTC Shinyanga ilibadilishwa na kuwa
Biashara Shinyanga.
Tatizo
lililotokea ni ubinafsi na watu wote wa Tanzania kuamini unapokuwa shabiki wa
soka, eti lazima upende Yanga au Simba, kitu ambacho ni sawa na kutumia hoja
chakavu ili kutetea jambo la msingi.
Wananchi wa
mikoani walikosa uzalendo na nguvu zao wakazielekeza kwenye ushabiki wa Simba
na Yanga ambazo hazitokei mikoani walipo wenyewe.
Leo watu wa
Mbeya wamebadilika, wamezinduka na wanaonyesha upendo unatakiwa kuanzia
nyumbani, wanaipenda kwa dhati na kuiunga mkono timu yao ya Mbeya City.
Mbeya City
ndiyo imepanda daraja hadi Ligi Kuu Bara lakini sasa inatoa ushindani mkubwa
kwa kuwa inapata sapoti kubwa sana. Angalia mechi ya juzi ya Mbeya ‘derby’
dhidi ya Prisons, Uwanja wa Sokoine ulijaa utafikiri ni Simba na Yanga.
Wengine
katika mikoa kama Mwanza, Arusha, Shinyanga, Rukwa na kwingine, wala msione
aibu kufuata wanachofanya watu wa Mbeya kipindi hiki. Siwaungi mkono kwa zile
vurugu zilizotokea baada ya mechi dhidi ya watani wao Prisons, lakini
wanastahili sifa kwa kuiunga mkono timu nayo.
Mkoa mzima
kutokuwa na timu hata moja katika ligi kuu au daraja la kwanza ni aibu kubwa,
hasa kwa mikoa ambayo ina historia ya juu kuhusiana na soka. Mfano Mwanza,
Kigoma, Dodoma, Iringa na Morogoro ambayo pamoja na kuwa na Mtibwa Sugar
inastahili kuwa na Moro City au Moro Municipal.
Najua ninawaudhi
lakini lengo ni kuwakumbusha kwamba, kuna kila sababu ya kuukuza mpira nchini
kwa kuwa na timu nyingi bora kutoka katika maeneo mengi.
Hakuwezi
kuwa na maendeleo kwa kila Mtanzania mpenda soka kushangilia Simba au Yanga
pekee na kama ni uzalendo, basi uanzie sehemu mnazotokea.
Zisaidieni
timu zenu kwanza na Yanga na Simba mnaweza kuzishangilia pia, lakini wahusika
wakuu wa klabu hizo kongwe ni watu wa Ilala na Dar es Salaam kwa jumla.
Inawezekana
mwanzo mlipuuzia kuhusiana na hilo, Mbeya City na wananchi wa Mbeya
wamewazindua na kuwaonyesha kwamba inawezekana. Kitu kizuri ni hiki, kuiga
maendeleo si dhambi, hivyo mnaweza kuwafuata kwa kukimbiza mgongo wao ili
kuleta mabadiliko katika soka.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment