Hapa nyumbani suala la waamuzi kulaumiwa sana linakua kila kukicha, ajabu kila
mwamuzi anayeingia kwenye mgogoro wa namna hiyo siku chache baadaye hupotea.
Mwamuzi
anayebainika kuwa ameharibu, baada ya siku chache hupotea kabisa, labda aibuke
baadaye sana. Huenda kuna kitu cha kujifunza kwa waamuzi wa Ligi Kuu Bara kwani
mambo ni tofauti kwa Howard Webb ambaye anaonekana ni wa aina yake, kwani
pamoja na lawama nyingi kila kukicha, kama utazungumzia mwamuzi mahiri zaidi
katika Ligi Kuu England, hakika hautamkwepa Webb.
Webb
ndiye mwamuzi mwenye mafanikio zaidi nchini humo kwa kipindi hiki, lakini ndiye
anaongoza kwa kulaumiwa zaidi kuliko mwingine yeyote.
Hata
kimataifa, yeye ndiye mwenye mafanikio makubwa na mfano mzuri ni mwaka 2010
alipopewa nafasi ya kuwa mwamuzi bora duniani, kwani ndiye alishika kipenga
wakati wa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania waliochukua ubingwa na Uholanzi.
Kama
hiyo haitoshi, inaonekana yeye ndiye anaaminiwa zaidi katika fainali mbalimbali
kubwa na maarufu kama ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2010, Kombe la FA
2010 na 2006 na Kombe la Ligi 2007 na
ndiye anaongoza kwa kupewa mechi zinazoonekana zina ushindani zaidi
Premiership.
Hata
hivyo, Webb amekuwa akiambiwa apunguze kumwaga kadi kama njugu, hasa za njano,
tena amekuwa akifanya hivyo huku akicheka.
Baadhi
ya makosa amekuwa akifanya na kukubali kuwa aliboronga, lakini kwingine
anashikilia msimamo wake. Mambo ni mengi, baadhi wamekuwa wakisema ni shabiki
mkubwa wa Manchester United.
Askari:
Alikuwa
askari polisi wa cheo cha sajenti kabla ya kuamua kuachana na kazi hiyo na kuwa
mwamuzi. Hali yake ya kujiamini sana inaelezwa inatokana na mafunzo yake ya
uaskari.
Baba:
Baba
yake mzazi, Billy Webb, alikuwa ni mwamuzi mahiri kwa
kipindi cha miaka 35 na alikumbana na kashkash kibao kama zile anazopata
mwanaye katika kipindi hiki.
Man United:
Amekuwa akisisitiza yeye si shabiki wa Man United na wengi kuamini
anaishabikia timu hiyo, ilitokana na Kocha Alex Ferguson kumtetea kuhusiana na
uamuzi wake wa kuipa timu yake penalti ambayo wengi walikuwa wanaipinga.
Yeye ni shabiki wa timu inayojulikana kwa jina la Rotherham United ambayo imekuwa ikishiriki
ligi za chini kama daraja la kwanza, la pili, tatu na mengine.
Webb amekuwa hajifichi kuhusiana na ushabiki wake katika timu hiyo ambako
ndiko alizaliwa na siku zote amekuwa akisisitiza yeye na Man United ni vitu
viwili tofauti.
Nje:
Nje ya
soka, Webb ana maisha yake, ameoa, baba wa watoto watatu na amekuwa akionekana
mara kadhaa na familia yake katika sehemu mbalimbali, hali inayoonyesha ni baba
bora.
Juni
2011, Webb alipewa urais wa Ligi ya Baris Northern Counties East ambayo aliwahi
kufanya kazi kama mwamuzi pia.
Ana
digrii ya udaktari aliyopokea katika Chuo Kikuu cha Bedfordshire na digrii
nyingine ya heshima ya masuala ya sayansi ya afya aliyoipokea katika Chuo Kikuu
cha York St John.
Makosa:
Moja:
Webb
ana makosa yake kama binadamu wengine, lakini yako kadhaa ambayo hayatasahaulika
kama lile la mwaka 2009 alipochezesha fainali ya Kombe la FA kati ya Man United
na Tottenham.
Wakati
Spurs wakiongoza kwa mabao 2-0, alitoa penalti ya utata kwa Man United ambayo
ilisaidia kuamsha nguvu ya vijana wa Ferguson na kuwashusha Spurs ambao mwisho
walipigwa 5-2 na United wakawa mabingwa.
Kweli
baadaye alikiri kuwa alichofanya hakikuwa ni sahihi na aliipa United penalti
kwa mizengwe akiamini kuwa ilikuwa ni sahihi kumbe siyo.
Mbili:
Mapema
mwaka 2009, Webb aliugonga mpira uliopigwa na Radhi bila ya kutegemea ukamfikia
Michael Kightly wa Wolverhampton aliyetoa pasi nzuri iliyozaa bao la pili na
kuimaliza Birmingham.
Katika
mechi hiyo, tayari kipindi cha kwanza alitoa penalti isiyo sahihi baada ya
Marcus Bent kuanguka katika eneo la hatari lakini haikuwa hivyo. Akakubali
lilikuwa ni kosa.
Birmingham
walipoteza mchezo huo na ikaonekana tatizo ni hilo bao la pili ndilo lililowaua
na kosa la Webb lililaumiwa hata na waamuzi wengine kwamba mwamuzi anapaswa
kuwa makini kuepuka kuingilia mchezo.
Tatu:
Februari
2012 alitoa penalti kwa Manchester United ikasawazisha katika mechi yake dhidi
ya Chelsea na matokeo yakawa 3-3. Kocha wa Chelsea wakati huo, Andre Villa Boas,
akalalama na kusema Webb aliwauma.
Ikaonekana
kama kocha huyo alikuwa na jazba kama ilivyozoeleka, lakini mwisho uchunguzi
ukaonyesha United hawakustahili kupata mkwaju huo.
TAKWIMU ZA WEBB MSIMU HUU:
MECHI 30
NJANO 110
NJANO YA PILI 0
NYEKUNDU 4
0 COMMENTS:
Post a Comment