November 26, 2013





Palikuwa hapatoshi katika viwanja vya burudani vya Leaders Club jijini Dar es Salaam pale wasanii mahiri mapacha Peter na Paul Okoye alimaarufu kama P Square kutoka nchini Nigeria walipozikonga vilivyo nyoyo za mashabiki kwa takribani muda wa masaa matatu mfululizo jukwaani. 
 
Tamasha hilo ambalo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ya Jumamosi 23 Novemba, ilikuwa haijawahi kutokea nchini kwani mashabiki wamekiri uwezo wa kutumbuiza jukwaani pamoja na kutumia ala mbalimbali za muziki na wasanii hao ni wa hali ya juu.
Tamasha lilikuwa lenye kuburudisha sana kwani usalama ulikuwepo wa kutosha kitu ambacho wengi tulikifurahia, alisema bwana Rajabu Abdallah, mmoja wa mashabiki waliohudhuria usiku huo.


“Pongezi zangu za dhati nazielekeza kwa wadhamini wa tamasha hilo,Vodacom Tanzania,kwa kufanikisha ujio wa wasanii hawa na kubuni njia mbadala ya M-PESA kwa mashabiki kuweza kukata tiketi bila usumbufu wowote”kwa raha zetu”siyo kama miaka ya nyuma foleni na adha za wizi kwenye foleni ungetokea.Nawaomba wasife moyo waendelee kufanya hivyo kwani sio tu, wanatoa burudani kwetu mashabiki wa muziki bali wanawapa fursa wasanii wetu kujifunza kutoka kwa wenzetu wenye uzoefu wa kimataifa na pia sifa kwa nchi yetu kwani dunia nzima ilikuwa ikifahamu P Square wanafanya tamasha kubwa la muziki nchini.” Aliongeza Abdallah.


Rashid Nassoro alikuwa pia ni mmojawapo wa mashabiki waliokuwepo kwenye viwanja hivyo ambapo amesifia usalama wa hali ya juu uliokuwepo ndani na nje ya tamasha kwani hakukuwa na malalamiko ya aina yoyote ya mtu kufanyiwa kitendo chochote cha uhalifu.

“Mara nyingi tumekuwa na hofu ya vibaka ambao wamekuwa wakitishia usalama wetu kiasi kwamba tumekuwa tukiacha vitu vyetu vya gharama kama vile simu na fedha nyumbani kwa kuhofia kuibiwa na hivyo kupunguza idadi ya wengi kuja  kuhofia usalama wao na mali zao. Lakini katika tamasha hili hali imekuwa ni kinyume na tulivyotarajia kwani mashabiki na wakazi wa maeneo ya karibu wameonesha ustaarabu na ukomavu wa juu katika kuelewa ni nini maana ya watu kujumuika na kufurahi kwa pamoja bila la uvunjifu wa amani,  alimalizia Nassoro. 

Wakati huohuo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twisa amesema kwamba wao kama wadhamini wa tamasha hilo nchini wamefurahishwa na ushirikiano waliouonesha kufanikiwa kwa tukio hilo la kihistoria katika tasnia ya burudani nchini.
“Tamasha hilo limekuwa lenye mafanikio kwetu kwani hali ya utulivu iliyojitokeza siku ile ni dhahiri kwamba watanzania sasa wanaelewa nini maana ya burudani, na hii inazidi kutupa moyo wa kuzidi kudhamini matamasha mengi kadri tuwezavyo na tunaahidi kufanya hivyo.”
Wingi wa mashabiki waliojitokeza siku ile inaonesha ni jinsi gani tunakubalika na kuungwa mkono, Vodacom siku zote utabaki kuwa mtandao unaowajali wateja wake katika Nyanja zote na si huduma na bidhaa wanazozitoa, kwa niaba ya kampuni ningependa kuwashukuru sana Serikali kwa kuweka usalama wa hali ya juu,Pia na watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kwa ustaarabu mliouonesha siku ya tukio, na hilo imedhihirisha kweli nchi yetu ni kisiwa cha amani na utulivu.” Alimalizia Twisa.

Mbali na P Square katika tamasha hilo, pia wasanii nguli wa bongo flava Profesa Jay, Lady Jay Dee, Ben Pol pamoja na Joh Makini walidhihirisha kwa umati wa mashabiki waliokuwepo viwanjani hapo kwamba kiingilio chao hakikuenda bure. Wasanii hao waliipeperusha vilivyo bendera ya muziki wa Tanzania kwa wakali hao wa Nigeria kwamba hata sisi tunaweza kufanya makubwa tuwapo jukwaani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic