Washambuliaji wawili wa Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta na
Mrisho Ngassa ndiyo tishio zaidi kwa kikosi cha Kenya, Harambee Stars.
Stars itaikaribisha Harambee, Jumanne ijayo katika mechi ya kirafiki
itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Harambee Stars, Adel Amrouche ambaye anasifika kwa soka
la mipango, amesema Samatta na Ngassa wanapaswa kulindwa vema.
“Unapokutana na kila timu lazima uangalie uimara wa wapinzani wako uko
wapi na kipi cha kufanya. Siwezi kukataa kuhusiana na ubora wa Samatta, pia
Ngassa. Najua mengi sana kuhusu Tanzania lakini ni suala la kulifanyia kazi,”
alisema Amrouche, raia wa Ubelgiji na kuongeza:
“Pia ninajua kuna Thomas (Ulimwengu) na wengine, hivyo ni kazi ngumu
ambayo inahitaji hesabu. Kweli ni mechi ya kirafiki lakini najua kila upande
utataka kushinda.”
Tayari wachezaji wa kimataifa wa Kenya wapo jijini Nairobi, akiwemo
Victor Wanyama anayekipiga Southampton ya England na Denis Oliech anayeitumikia
Ajaccio ya Ufaransa.
Nyota mwingine wa Harambee ni kiungo wa Inter Milan, McDonald Mariga
anayekipiga Parma kwa mkopo, hajaitwa katika kikosi hicho cha Amrouche maana
hakuwa fiti lakini kiungo Mohammed Jamal anayekipiga nchini Oman tayari yupo
Nairobi kujiandaa na mechi hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment