November 1, 2013



Na Saleh Ally
Kiu ya wadau wa mchezo wa soka nchini kutaka kujua nani ni rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sasa imepata kipoozeo.


Imeishajulikana kuwa Jamal Malinzi ndiye atachukua nafasi ya Leodeger Tenga ambaye hakuna ubishi, amejitahidi kadiri ya uwezo wake kusukuma mambo mbele wakati wa uongozi wake wa miaka minane.

Pamoja na hivyo, bado kuna upungufu wa mambo mengi sana katika maendeleo ya mchezo wa soka kama vile vifaa ambavyo ni viwanja, mipira lakini walimu ambao wameelimishwa vizuri ili kuweza kuwasaidia vijana.

Mara baada ya kutangazwa mshindi kwa kumuangusha Athumani Nyamlani kwa kura 73 (57.9%) kwa 52 (41.2%), Championi Ijumaa lilitaka kusikia kauli ya kwanza ya Malinzi baada ya zile za kampeni kwa kuwa sasa atakuwa anazungumza akiwa ndiye Rais wa TFF na si mgombea kama ilivyokuwa mwanzo.

Malinzi anasema vitu muhimu vinavyohitajika katika mpira ili maendeleo yapatikane ni vipaji, walimu, vifaa na usimamizi wake unatakiwa uwe wa karibu.

“Katika usimamizi huo, lazima kuwe na watu ambao ni makini na wenye uchungu wa kutaka maendeleo katika kila nyanja.

“Maendeleo ya mpira yanajumuisha sehemu nyingi sana, mfano makocha wanaofundisha vijana, lazima waipende kazi yao kwa kuwa lazima kutakuwa na ugumu unaojitokeza, tusitegemee kila kitu kwa ulaini tu badala yake lazima tupambane.

Muda:
Lazima nitakuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu. Nitayagawanya mambo katika makundi hayo mawili na yako ya kushughulikia haraka kama mechi ya marudiano ya timu ya under 20 ya wanawake, Afcon na mingine.
Kwenye mipango ya muda mrefu, hii ndiyo itahusisha vitu vingi kama vijana na mabadiliko kwa jumla kuhusiana na mpira wetu.

Kujituma:
Katika mafanikio, suala la kujituma halikwepeki, wakati tunatafuta maendeleo vikwazo havikosekani. Maana yake lazima tuwe na watu wenye nguvu ya kutokata tamaa au kutanguliza lawama badala yake kuungana pamoja na kupambana.

Mabadiliko yanatakiwa kuwa makubwa sana, inawezekana tulichelewa lakini kwa kuwa uongozi wangu sasa umeingia madarakani, basi ndiyo wakati mwafaka wa kuanza kupambana ili kuleta mabadiliko.

Upendo:
Maendeleo yakipatikana, basi inayofaidika ni Tanzania. Lazima tuipende nchini yetu na ndiyo itakuwa rahisi kusaidia kupatikana kwa maendeleo. Tukiunganisha nguvu yetu sote na kuwa kitu kimoja hata kufikia mafanikio itakuwa rahisi.

Lakini kama kuna wengine wamegawanyika, basi huenda tutafanikiwa kwa shida sana au kujichelewesha. TFF kazi yake ni kusimamia maendeleo na kuongoza ipi ni njia sahihi, lakini kama watakuwepo ambao hawakubaliani na kila kitu, itakuwa kazi ngumu zaidi na tutachelewesha mambo mengi sana.

Serikali:
Bado ninaamini serikali ni mdau wa karibu wa michezo nchini, hivyo iingie na kusaidia maendeleo ya mpira katika sehemu ambayo inaamini inastahili kufanya hivyo.

Msaada wa serikali ni kitu muhimu, naendelea kuheshimu sana mchango wa serikali katika mchezo wa soka, lakini ninaamini unawezekana ukaongezeka na kuwa mkubwa zaidi ya hapa. Safari hii ni ndefu yenye milima na mabonde, serikali inaweza kuwa mwelekezaji mzuri wa njia sahihi kama ikiwa tayari kusaidia.

Vipaji:
Tunahitaji mambo mengi, kujenga vituo vya watoto, kuwafundisha makocha wetu na mambo mengine, ndiyo maana nikasema serikali ni mdau muhimu wa mchezo huu.
Hatuwezi kumuepuka, lazima tushirikiane kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya soka. Utaona serikali inapambana kutanua wigo wa ajira, soka inaweza kuwa moja ya sehemu nzuri ya kuitumia kutanua wigo wa ajira kwa vijana na Watanzania kwa jumla.

Mafunzo:
Nasisitiza sana mafunzo husika kwa kitu sahihi, mfano kuwa na walimu ambao wamesomea kufundisha watoto, hawa wanakuwa na mafunzo tofauti na wenyewe wanajua wafanye nini ili kuwakuza wachezaji.
Hawa wanakuwa na uwezo wa kutoa elimu na mafunzo ya michezo na mwisho tunakuwa na wachezaji ambao wanaweza kusaidia maendeleo ya soka ya ushindani, waelewa na wanaoweza kupambana na ushindani wa kimataifa.
Mashuleni:
Lengo kuwa na ligi za mashule kama ilivyokuwa awali, wachezaji wengi wameibukia katika michuano ya mashule. Mfano Mtemi Ramadhani na hata Leodeger Tenga kama sikosea.
Zamani mchezaji alikuwa anatokea shule moja kwa moja hadi timu ya taifa na Tanzania ilifanya vizuri. Hii ilitokana na mfumo imara wa kuendeleza wenye vipaji tokea wakiwa shuleni, lakini baadaye ikabadilika na wachezaji wakaanza kutokea vyuoni.

Lakini sasa ni nadra hata kusikia kuna mchezaji kutoka chuo kikuu fulani kaitwa timu ya taifa. Lazima tubadilishe mambo, lazima tujiandae lakini kwa kuhakikisha tuna hazina ya kutosha.

Timu ya taifa ya Zambia, mwaka 1993 ilipata ajali ya ndege na wachezaji wote wakapoteza maisha, mwaka uliofuata waliingia katika Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, wakafika hadi fainali na kufungwa na Nigeria.

Utajiuliza kwa nini kama timu nzima ilipotea lakini kipindi kifupi baadaye wakaweza kufanya vizuri hata kuliko timu nyingine ikiwemo Tanzania ambayo hata kuingia tu katika fainali hizo imebaki historia? Sisi tukikosa wachezaji wawili, timu inapoteza dira, lakini tukubali tunahitaji hazina ambayo inapatikana kwa maandalizi na michuano iliyo bora katika program bora na mashindano ya shule, litakuwa jibu sahihi.

Wadau:
Maendeleo ya soka bila ya fedha itakuwa ni kazi bure, niseme wazi ninahitaji fedha na hili ni jambo muhimu duniani kote.
Hivyo makampuni ambayo yana uwezo wa kuingia na kudhamini mchezo wa soka wafanye hivi, katika kipindi chetu mambo yatabadilika.

Wadhamini ligi za vijana na mambo mengine muhimu kwa kuwa kama watafanya hivyo, mpira utazidi kukua na wenyewe watapata matokeo mazuri katika kutimiza lengo la kukitangaza wanachotaka kitangazwe.

Muda:
Hili ni muhimu sana, mambo ya kurekebishwa ni mengi na kila jambo linahitaji muda, ninakuhakikishia tutapambana sana. Lakini kuna mambo mawili muhimu, Watanzania lazima wakubali uongozi wetu utakuwa unahitaji muda katika utekelezaji.

Pili watu wasijitenge, tuungane pamoja na tuamini kama ni matatizo ya mpira yawe ya wote na siku tunafurahi, tufurahi pamoja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic