Mpachika mabao wa Simba, Amissi Tambwe, amesema timu yao
inahitaji kuongeza kiungo na winga mmoja kwenye usajili wa dirisha dogo.
Usajili huo wa dirisha dogo ulifunguliwa Ijumaa iliyopita na
unatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu.
Tambwe amesema nafasi hizo
ndizo zenye upungufu na kwamba ndizo zilizosababisha kushindwa kutimiza idadi
ya mabao aliyopanga katika mzunguko wa kwanza wa ligi.
Tambwe alisema katika mzunguko wa kwanza, amefunga bao moja
pekee la kichwa kutokana na timu yao kukosa winga mwenye uwezo wa kupiga krosi
nzuri za kufunga.
“Ujue katika mabao yangu kumi niliyofunga kwenye mzunguko wa
kwanza wa ligi, yote nilifunga kwa mguu, kwa njia ya pasi, isipokuwa moja pekee
nililofunga kwa kichwa.
“Nimeshindwa kufunga kwa kichwa kutokana na timu kukosa
mawinga wenye uwezo wa kupiga krosi, hivyo ili niendelee kufunga mabao kwenye
mzunguko wa pili wa ligi, basi viongozi wasajili winga na kiungo mwenye uwezo,”
alisema Tambwe.
Mshambuliaji huyo anaongoza kwa mabao kwenye ligi kuu akiwa
na 10, akifuatiwa na Elius Maguri wa Ruvu Shooting aliyefunga 9 na Hamis Kiiza
wa Yanga mwenye 8.
0 COMMENTS:
Post a Comment