December 23, 2013





3-1 ilizopigwa Yanga ni fundisho kwa wote waliokuwa wamelala
SIMBA wanastahili pongezi kutokana na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya watani wao wa jadi Yanga ambao walionekana watashinda mechi hiyo ikiwezekana kwa mabao mengi.
 
Ushindi wa Simba una mambo mengi sana ya kujifunza na wakati mashabiki na wanachama wake wanashangilia, basi wapiti mambo kadhaa ambayo ni muhimu.
Kujifunza si kwa mashabiki na wanachama wa Simba pekee, badala yake hata wale wa Yanga na timu nyingine lakini kwa viongozi mfano wa Mwenyekiti wa Simba aliyesimamisha, Ismail Aden Rage pia anaweza kuona namna kamati ya utendaji ilivyosimamia maandalizi ya timu katika mechi hiyo.
Kikubwa zaidi cha kujifunza ni mambo makuu mawili, dharau na nia ya dhati ya kutaka kukifanya kitu fulani kwa ajili ya mafanikio.
Tunaweza kudanganyana sana lakini hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana bila ya kujitolea, hata kama utakuwa na akili kuliko za mchwa, linapofikia suala la kutafuta na kupata mafanikio, kujitolea ni lazima.
Yanga walikuwa na kila kitu na hakuna ubishi, kikosi chao ni bora kuliko kile cha Simba, hali hiyo iliwafanya waone kila jambo linawezekana tena kwa ulahisi, wakaingia uwanjani na matokeo yakiwa vichwani kabla hata ya kuucheza mpira.
Ninaamini kilichowatokea wamekiona, lakini Simba walijua wanachukuliwa ‘poa’, wakafanya maandalizi na kuipa uzito mechi hiyo mwisho wamepata ushindi mkubwa ambao unastahili pongezi.
Simba hawakupata ushindi wa mabao pekee, hata soka wameonyesha bora na la kuvutia, wamegeuza mambo, wamegeuza hisia na sasa wanastahili kuitwa kikosi bora kama tathmini itakuwa ni mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe.
Pili  ni suala la nia, yaani kujitoa kwa ajili ya kitu. Hata kama mtabisha, Watanzania wengi tumekuwa ni watu wa kusubiri ahadi ili tuweze kutekeleza kazi zetu kitu kinachotuingiza kwenye kundi la “on off”, kwamba kuwasha taa lazima utumie ‘swichi’.
Jiulize mtu anayelipwa mshahara vipi analazimika kupewa ahadi ili afanye kazi yake vizuri, kwa nini asifanye kazi vizuri halafu motisha ifuatie. Suala hilo linawezekana mara mojamoja lakini lisiwe wajibu na lazima.
Mtu anayependwa kuahidi kitu ndiye ajitume kila mara, lazima atakuwa na tatizo. Wanaofanikiwa ni wale wanaojitambua, wanajituma kufikia ndoto zao na si kusubiri kuzawadiwa ili wafikie mafanikio.
Mwisho mzigo utamuangikia kocha au benchi la ufundi, mara nyingi hilo halina mjadala. Lakini ukweli unabaki kwamba hata wachezaji walikuwa tatizo kwa kuwa walitanguliza dharau, wakasahau kazi. Wao pia wajifunze kwamba hata uwe na uwezo vipi, kazini lazima ujitume.
Lakini mwisho kwa mashabiki waliokwenda uwanjani kuzishangilia timu zao pia nao watakuwa wamepata somo na hawatakiwi kusahau hili, zaidi naona linawagusa wale wa Yanga.
Mpira si maneno mengi mdomoni, matokeo ya mchezo hupatikana baada ya mechi. Hivyo si vema kwenda uwanjani mkiamini mmeshinda na inapotokea mmefungwa hata kama ni hali, basi lazima kuwe na wa kumlaumu au kuamini mmeonewa.
Uzuri wa mechi ya juzi, hakuna shabiki hata mmoja hasa kwa wale wenye tabia ya kutafuta wachawi aliyepata nafasi ya kuinua mdomo na kumlaumu mwamuzi kwa kuwa mabao yote yalikuwa safi kabisa.
Kawaida lazima kuwe na mchawi, lakini bado somo linaendelea kwamba ndiyo maana mashabiki wanakwenda uwanjani kuangalia kitakachotokea kwa kuwa dakika 90 ndiyo utabiri sahihi katika soka.
Yanga walikwenda uwanjani wakiwa wameishaifunga Simba, walichotaka kujua ni bao ngapi na hilo lilikuwa kosa kubwa. Soka linapendwa zaidi duniani kwa kuwa matokeo yake hayana mwenyewe.
FINITO.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic