Na Waandishi Wetu
UNAIKUMBUKA sare ya maajabu ya mabao 3-3
ya Oktoba 20, mwaka huu? Sasa hiyo cha mtoto, kesho ndiyo kesho kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam, wababe hao wa Tanzania wanakutana kwa mara nyingine
kwenye dimba hilohilo katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
Mengi yanazungumzwa lakini machache
ambayo ni gumzo ni Emmanuel Okwi kuruhusiwa na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kuichezea Yanga katika mtanange huo, huku Kocha wa Simba, Zdravko
Logarusic akisema Okwi ambaye ametua jana jijini, kwake siyo tatizo na kudai
dawa yake ipo na amewataka mashabiki wa Simba wasiwe na hofu hata kidogo.
Okwi
atua aruhusiwa kucheza
Okwi alitua jana majira ya saa kumi
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, ambapo
alipokewa na umati mkubwa wa mashabiki wa Yanga wengi wao wakiwa wamevaa jezi
za njano zenye jina la Okwi, huku wakiimba “Rage bado Kapombe, Rage bado
Kapombe.”
Alipowasili ilibidi apitishiwe mlango wa
watu maarufu ‘VIP’, akiwa amevalishwa jezi yenye namba 25, Okwi alizungumza machache
kwa kusema: “Nawashukuru Simba kwa kipindi chote tulichokuwa pamoja, nimerejea
Tanzania kuja kufanya kazi na ninaamini mechi ya Jumamosi timu yangu ya Yanga
itaibuka na ushindi.”
Wakati akitoka uwanjani hapo ilibidi
askari polisi waongezeke kumlinda kutokana na mashabiki wengi kugombania
kumsalimia kwa kumgusa na kumkumbatia.
Upande mwingine, Mkurugenzi wa
Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, ameliambia gazeti hili kuwa, wamepokea
pingamizi la kumzuia Okwi kutoichezea Yanga kutoka kwa Mwenyekiti wa Simba,
Ismail Aden Rage, juzi lakini akasisitiza Yanga ikiamua kumtumia ni ruksa.
“Hakuna kitu kinachoitwa ITC feki, ITC
ikitoka imetoka, hilo watu wanatakiwa kujua, tumepokea pingamizi la Rage kuhusu
Okwi. Rage ametumia haki yake ya kidemokrasia kuwasilisha pingamizi kwa kuwa
tupo katika kipindi cha mapingamizi kinachomalizika Desemba 23.
“Kuhusu Okwi kucheza Jumamosi hakuna
tatizo kwa kuwa mechi hiyo siyo ya kimashindano, unakumbuka (Mrisho) Ngassa
aliichezea Seattle Sounders ya Marekani dhidi ya Manchester United licha ya
kuwa alikuwa ni mali ya Azam FC, kumtumia au la huo ni uamuzi wa Yanga,”
alisema Kawemba.
ITC ni Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
ambayo inamruhusu mchezaji kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine katika nchi
tofauti.
Simba
kutumia mifumo mitatu
Loga amesema ana mifumo mitatu
atakayoitumia kuwamaliza Yanga lakini akagoma kuitaja ili Kocha wa Yanga, Ernie
Brandts asijue janja yake na kuitegua. “Nimepanga kutumia mifumo mitatu tofauti
katika mechi moja, sitakutajia kwa kuwa nitakuwa najimaliza mwenyewe,” alisema.
Vita
ya Berko, Ivo ni ngumu
Inaelezwa kuwa, Loga bado hajafanya
uamuzi wa kipa wa kumtumia na kuwa chaguo la kwanza kati ya Yaw Berko na Ivo
Mapunda ambao wote wametua klabuni hapo hivi karibuni.
Loga amesema: “Ninahitaji muda zaidi wa
kuangalia uwezo wa kila kipa akiwa golini kabla ya kuamua yupi anafaa kuwepo
kwenye kikosi changu cha kwanza nitakachokitumia kwenye mzunguko wa pili.”
Yanga
bado waota sare ya maajabu
Beki wa Yanga, Mbuyu Twite amesema Simba
wasitarajie kupata mchekea wa kusawazisha mabao kama ilivyokuwa katika mechi ya
3-3, licha ya Yanga kuongoza kwa mabao 3-0 mpaka mapumziko.
“Simba wasitarajie kuwa tutarudia makosa
ya mechi iliyopita ya kuwafunga mabao matatu na baadaye wanarudisha yote,
kiukweli wasahau hilo,” alisema.
Chollo,
Telela waondolewa
Kiungo Salum Telela wa Yanga na beki wa
Simba, Said Masoud ‘Chollo’ kwa nyakati tofauti wameondolewa katika timu zao na
hawatakuwepo kwenye mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi.
Eti
Okwi alikuwa tishio kwa Cannavaro!
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ amefunguka kuwa Okwi ndiye mchezaji pekee aliyekuwa akimsumbua
wakati alipokuwa Simba.
“Niseme ukweli nimepokea kwa furaha sana
taarifa za ujio wa Okwi, katika maisha yangu ya soka Okwi alikuwa akinisumbua
kila nilipokuwa nikikutana naye lakini sasa presha hiyo sina tena, nawapongeza
sana viongozi wa klabu waliofanikisha hili,” alisema Cannavaro.
Wachezaji
‘full’ tambo
Jerry Tegete wa Yanga: “Tumejipanga
vizuri kuhakikisha tunapata ushindi, kutokana na maandalizi ya nguvu
tunayofanya na kocha wetu.”
Juma Kaseja wa Yanga: “Sina hofu ya
mechi hiyo kutokana na uzoefu mkubwa nilionao wa kuzichezea timu hizi mbili.”
Amissi Tambwe wa Simba: “Kesho mpaka
kieleweke, ushindi ndiyo lengo letu, tuna maandalizi mazuri.”
Ivo Mapunda wa Simba: “Nitazingatia kile
kilichonileta Simba ili niweze kufanya vizuri na kitu cha msingi cha
kuzingatiwa ni ushirikiano kutoka kwa wachezaji, viongozi na wanachama kwa
jumla.”
Didier Kavumbagu wa Yanga: “Unapohitaji
kufunga hauna sababu ya kuangalia nani anakukaba au anayedaka, kwa hiyo uwepo
wa Berko haunitishi.”
Yanga
wajifua kwa penalti, mashuti
Kikosi cha Yanga, jana kilikuwa katika
mazoezi makali lakini cha kuvutia katika mazoezi hayo ni upigwaji wa penalti na
mashuti makali katika Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini.
Kaseja alifungwa mashuti 18, akaokoa 11,
akiteswa zaidi na Nizar Khalfan wakati Barthez akifungwa mashuti 21, akiokoa
10, akiteswa na Didier Kavumbagu na Hussein Javu.
Tegete alikuwa kinara katika penalti kwa
kumtesa Kaseja, ambapo jumla Kaseja alifungwa mikwaju nane huku akipangua
penalti za Athuman Idd ‘Chuji’, Mrisho Ngassa huku Barthez akicheza nne.
0 COMMENTS:
Post a Comment