Na Saleh Ally
JUZI Jumatano, Mzee Small alieleza namna alivyoshindwa kuvumilia na
kumtimua mganga aliyekuwa akimtibu tena kwa kumshikia panga, hali hiyo
ilitokana na wao kutoelewana. Nini kilifuata baada ya hapo?
Endelea na Mzee Small…
HATA hivyo haikuwa kazi rahisi Mzee Small kumfukuza mganga huyo kwa
kuwa mkewe Mama Said alijaribu kumshawishi angalau avumilie kidogo.
“Mganga alimueleza mke wangu kwamba nilikuwa nimechanganyikiwa ndiyo
maana ilikuwa ni vigumu kwangu kumuelewa.
“Lakini mimi sikuwa nimechanganyikiwa, nilikuwa naelewa kila kitu na
kwa kifupi nilikuwa nimechoka kutokana na mambo yalivyokuwa yanakwenda.
“Mwisho nikashikilia msimamo wangu, kwamba ilikuwa lazima aondoke,
kweli ikawa hivyo na nikaamua kuendelea na matibabu mengine.
“Unaona kipindi hiki ninafanya mazoezi mara mbili kwa siku pale kwenye
hospitali ya hukuhuku Tabata. Kweli napata nafuu na unaona mambo yanakwenda
yanabadilika.
“Natamani sana kupona ili nirudi kufanya kazi yangu ya sanaa, naipenda
sana. Utaona hata yule kijana pale (anaelekeza kidole kwa mtoto wa ndugu yake).
Nilimuambia nikipona tu, basi nitaanza kumfundisha, naye amekuwa akisubiri.
“Unajua sanaa hii ndiyo imefanya nijulikane kwa watu wengi kila
sehemu. Sanaa hii ndiyo imenipandisha ndege na kunipeleka hadi Ulaya na
kwingineko.
“Nimesomesha wanangu kupitia kazi hii, wengine wamefika hadi vyuoni
ambako sijawahi kufika, lakini ni hiihii sanaa ya uigizaji ndiyo maana
naiheshimu sana,” anasema Mzee Small akionyesha kujiamini.
“Achana na kuwasomesha wanangu na kuilea familia kwa jumla, lakini
ninaipenda sana. Wakati mwingine ukifanya kitu, lazima ukipende.
“Pia sanaa hii imenikutanisha na watu wengi wakubwa, mfano Rais
Kikwete amekuwa rafiki yangu miaka mingi sana tokea akiwa kiongozi wa Umoja wa
Vijana wa CCM.
“Baadaye pia alivyokuwa waziri, tulikuwa tukizungumza mambo mengi
kuhusiana na sanaa na tulibadilishana sana mawazo. Natamani sana siku moja aje
anione.
“Najua kutokana na nafasi yake atakuwa amebanwa na majukumu mengi
sana, lakini akiweza kufika hapa siku moja na kuniona, basi nitafurahi sana.
“Sisemi hivyo nalazimisha, hapana ila kama ikitokea hivyo litakuwa ni
jambo zuri kwangu kwa kuwa yeye (Kikwete) ni rafiki yangu,” anasema Mzee Small
akionyesha kujiamini.
Mzee Small amekuwa akitembea kwa kujivuta kutokana na mwili wake
kuishiwa nguvu upande mmoja kutokana na kupooza.
Mara kwa mara amekuwa akieleza namna gharama za matibabu zinavyombana
kwa kuwa anashindwa kujiingizia kipato kutokana kulazimika kubaki nyumbani
tokea Mei, mwaka jana.
Lakini anasema hajakata tamaa na iko siku atarejea tena huku
akisisitiza, kwamba wako watu wamekuwa wakikunwa na kuumwa kwake.
“Wako wanakuja kuniona na wanaumia na kuumwa kwangu, yote hii ni
sanaa. Mimi sitaki kuingia kwenye kuwalaumu watu kutokana na kuumwa kwangu.
“Sanaa ni pana, bado naendelea kushukuru hapa nilipo na ninasema nina
mke bora ambaye ananiangalia vizuri maana wakati fulani hali yangu ilikuwa
mbaya sana.
“Ila bado nashukuru kwamba sanaa ya uigizaji imenilinda, imenipa watu.
Tena sijakuambia, wakati fulani nilikuwa na urafiki na marehemu Julius Nyerere
kutokana na sanaa hii na wakati ule kumkaribia hakikuwa kitu rahisi,” anasema
Mzee Small.
KUMBE Mzee Small aliwahi kuwa rafiki wa marehemu baba wa Taifa? Je, wakati
akiwa hai waliwahi kukutana mara ngapi, wapi na walizungumza nini? Fuatilia
JUMATATU.
0 COMMENTS:
Post a Comment