Sergio Kun
Aguero ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao katika Ligi Kuu England
inayoendelea kwa kasi kubwa.
Takwimu
zote zinazomhusu na zitakazozungumziwa hapa ni zile kabla ya mechi za ligi hiyo
dhidi ya Swansea ambayo imepigwa jana Jumapili.
Raia huyo
wa Argentina, pamoja na kuwa na mabao 10 ya kufunga, lakini takwimu za
kitaalamu zinaonyesha ndiye mchezaji aliyepiga mashuti mengi zaidi, amepiga mashuti
42. Anayemfuatia ni Luis Suarez (41) na Danny Sturridge (40), wote wa
Liverpool.
Ukirudi
katika kucheza dakika nyingi, Aguero ana dakika 838 kabla ya mechi hiyo ya jana
na anaingia moja kwa moja kwa washambuliaji watano waliocheza muda mwingi na kufanya
vizuri zaidi.
Huu si
msimu wa kwanza, tangu atue England akitokea Atletico Madrid msimu wa 2011-12,
ameisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa na amekuwa mmoja wa wachezaji nyota kwenye
kikosi hicho na kwenye ligi hiyo kwa jumla.
Aguero
aliweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi tangu Sheikh
Mansour alipoinunua Manchester City. Uhamisho wake ni ghali zaidi kuliko
mchezaji yeyote katika kipindi chote cha Mwarabu huyo.
Alihamishwa kutoka Atletico Madrid kwa kitita cha pauni
milioni 38, wengine waliomfuatia ni Robinho (pauni 32.5m), Edin Dzeko (pauni 27m),
James Milner (pauni 26m) na Carlos Tevez (pauni 25.5m).
Bado rekodi
zake akiwa Atletico Madrid zimekuwa bora na za kuvutia, hakuna ubishi tena hadi
sasa ni mmoja wa washambuliaji bora na wanaokwenda tofauti na mfumo wa Ulaya
kwamba mshambuliaji lazima awe mrefu na mwenye mwili mkubwa. Aguero si mrefu
sana kwa kuwa urefu wake ni futi 5 na inchi 8 tu, sawa na washambuliaji wengi
wa Ligi Kuu Bara.
Mafanikio
yote hayo ya Aguero hayakupatikana kirahisi hata kidogo, inawezekana kabisa akawa
changamoto kwa wachezaji wengi wa Bara la Afrika na hasa Tanzania ambako maisha
kwa asilimia kubwa ni shida.
Aguero
ameishi maisha ya shida, mabaya na makali kuliko Watanzania wengi ambao huenda
wanaona wana shida sana au Mwenyezi Mungu amewasahau, lakini aliweza kutoka na
kufikia alipo sasa.
Katika
kujaribu maisha, amepita kila sehemu hadi kuamua kuwa mwanamuziki, aliimba bila
ya mafanikio na mwisho akaamua kuushika mpira akiamini utamtoa, kweli ikawa
hivyo.
Miaka 25
iliyopita, mshambuliaji huyo ambaye jina lake halisi ni Sergio Leonel Agüero
del Castillo, alizaliwa katika mji mdogo wa Quilmes nchini Argentina na kukulia
katika viunga vya mji mkubwa Argentina wa Buinos Aires vinavyojulikana kama
Villa Itali.
Maisha
yalikuwa ni ya shida sana kwa kuwa baba yake mzazi alikuwa ni dereva taxi
ambaye alikuwa na uwezo wa kuingiza pauni 20 (Sh 50,000), fedha ambayo ilikuwa
haitoshi hata kidogo.
Baba yake
alikuwa akiondoka nyumbani alfajiri na kurejea saa 6 usiku, maisha yalikuwa ya
kubahatisha sana na magumu. Malezi ya wazazi ya kawaida hayakuwepo kwa kuwa
wazazi walilazimika kupambana kupata maisha.
Ugumu wa
maisha ulimlazimisha Aguero kuishi maisha asiyokuwa akiyataka kwa maana ya
mafanikio, alikuwa akikimbia kucheza soka na kwenda kwenye muziki kwa kuwa aliamini
watu walio upande huo wangekuwa wastaarabu kuliko wale wanaocheza soka.
Eneo la
Villa Itali lilikuwa na wakazi wanaofikia 60,000 tu, lakini inaelezwa nusu ya
wakazi wake walikuwa wanajihusisha na uuzwaji wa madawa ya kulevya na hasa wale
waliokuwa wakishiriki mchezo wa soka.
Wakati
fulani, Aguero alipoulizwa kuhusiana na maisha ya Villa Italli, alijibu kwa
kuonyesha anasikitika na neno la kwanza lilikuwa hivi: “Soka limeniokoa.”
“Hata
rafiki niliokua nao, nimeambiwa asilimia zaidi ya 90, hasa kwa wale waliobahatika
kuendelea kuishi, wapo gerezani. Yalikuwa maisha ambayo kila mmoja asingependa
kuyakumbuka. Kama nisingeondoka pale kwa sababu ya mpira, kweli hata sielewi
sasa ningekuwa ninaishi maisha gani.”
Kauli hiyo
ya Aguero ilifuta lawama ya Gazeti la The Sun la Uingereza lililotumia kichwa
cha habari cha Slumgold Millionaire, kuonyesha makazi duni aliyokulia, naye
akasisitiza wala haoni tatizo lolote kwa kuwa Villa Itali ndiko alikotokea.
Inawezekana
ni rahisi kwa wanasoka makinda waliokata tamaa kwa kuwa wanatokea katika
familia duni, wazazi wao ni watunza bustani, madereva taxi, bajaj au bodaboda
ambao walikuwa wakiamini hawawezi wakafanikiwa.
Aguero
aliamua kuepuka biashara ya madawa ya kulevya angalau kwa kiasi fulani na
kuingia katika muziki. Mara nyingi jioni alikwenda kujifunza kuimba na kipaji
chake kilikubalika.
Lakini
kila sehemu kuna wakatisha tamaa na mizengwe haina mipaka, alianza kuona baadhi
ya walimu na viongozi wa bendi aliyokuwa akiitumikia wakipendelea watu fulani.
Mwisho,
tena kwa hasira, akaamua kurejea kwenye soka, safari hii akiwa amepania kupata
mafanikio kwa kuwa alichoka maisha ya mlo mmoja kwa siku huku waliokuwa
wakifanya biashara ya madawa ya kulevya wakiishi kwa raha.
Kwa
kuwa wengi walikuwa rafiki zake, walijaribu kumshawishi lakini yeye akaapa kwa
kuwa muziki ulishindikana, siku moja atatoka kupitia soka.
Muziki
aliupenda kiukweli, ni shida tu ndizo zilimlazimu kuimba. Ndiyo maana hata
baada ya kupata mafanikio akiwa na timu ya Independiete iliyomkuza kisoka na
baadaye Atletico Madrid, aliamua kurejea katika muziki.
Aliimba
wimbo maarufu wa El Kun Aguero ulio katika
miondoko ya Cumbia, maarufu zaidi katika Bara la Amerika Kusini na hasa nchini
Colombia. Wimbo huo alioshirikiana na bendi moja maarufu, umekuwa ukiendelea
kupigwa hadi leo.
Tayari amefanya mambo mengi
makubwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba, kuwanunulia usafiri na
kuwafungulia biashara wazazi wake.
Zaidi amekuwa akitumia jina
la Kun alilopewa na babu na bibi yake kutokana na kuvutiwa zaidi ya katuni ya
kwenye runinga iliyokuwa maarufu kwa jina la Kunkun.
Aguero ni mkwe wa gwiji la
soka Argentina na duniani, Diego Armando Maradona, kwani alimuoa binti yake
Giannina ambaye alizaa naye mtoto Benjamin aliyezaliwa Februari 19, 2009. Hata
hivyo Januari 2013, Aguero na binti huyo mdogo kuliko wote wa Maradona,
walitengana.
0 COMMENTS:
Post a Comment