AL RAWAHI (WA PILI KULIA) AKIWA NA TALIB HILAL NA MALKIA WA NYUKI WAKIMSIKILIZA KOCHA WA ZAMANI WA SIMBA, PATRICK LIEWIG |
Na Saleh Ally
Jumatano iliyopita, Championi liliandika kuhusiana na
mwanachama mmoja wa Simba aliyeamua kumpa gari kiungo kinda wa Simba, Ramadhani
Singano ‘Messi’.
Juhudi za SALEHJEMBE hili zilifanikiwa kupata jina la
mwanachama huyo kuwa ni Musleh Al Rawahi aliyeonyesha upendo wa aina yake kwa
mchezaji huyo na klabu ya Simba.
Suala la Al Rawahi kutoa gari aina ya Suzuki Carry kwa
Messi lilipata mjadala mkubwa na wengi hawakuamini kama kuna mwanachama anaweza
kufanya hivyo tu.
Messi si mchezaji wa kwanza wa Simba au Yanga
kuzawadiwa gari, lakini kawaida wanachama au uongozi wa klabu hizo kubwa
huwazawadia wachezaji wake magari wanapokuwa wako katika harakati za usajili.
Ili kumvuta mchezaji, anapewa gari pamoja na fedha na
suala hilo limetokea mara nyingi sana mfano mzuri ukiwa ni ule wakati Mrisho
Ngassa akitokea Azam FC kwenda Simba, Kelvin Yondani akitokea Yanga kwenda
Simba.
Tofauti ya Messi na gari alilopewa si kipindi ambacho
kinajumuisha usajili, ni moyo tu wa kujitolea na mapenzi kwa klabu yake
aliouonyesha Al Rawahi!
Al Rawahi ni kati ya wajumbe wa kamati ya usajili ya Simba
hadi sasa na aliwahi kuwa kwenye kamati tofauti hapo kabla.
Wakati Simba chini ya Kassim Dewji ilipoing’oa Zamalek
mwaka 2003, Al Rawahi aliongoza kambi ya Oman kwa siku 10 kabla ya timu hiyo
kushuka Misri na kuivua ubingwa timu hiyo kigogo.
Juhudi za Championi kutaka kujua hasa Al Rawahi ni
nani, zimevumbua mambo kadhaa ambayo huenda hayakujulikana hapo awali na
yanaweza kuwa sababu ya kiongozi huyo kuamua kutoa gari hilo kwa Messi.
Al Rawahi si shabiki wa Simba leo au jana, amekuwa
akiipenda timu hiyo akiwa kinda na picha yake akiwa na kikosi cha Simba mwaka
1977 ndiyo inathibitisha hayo yote.
Kikosi hicho cha Simba ni kati ya vile bora kabisa
vilivyowahi kutokea katika historia ya klabu hiyo na Al Rawahi akiwa na umri wa
miaka sita pamoja na kaka Murshid (7) yake wako katika picha hiyo ya kikosi cha
Simba.
Kikosi hicho kilikuwa na wakali kama Aloo Mwitu,
Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Mohammed Kajole, Abdallah Mwinyimkuu na Daud Salim
‘Bruce Lee’.
Wengine waliokuwa katika kikosi hicho ni Martin Kikwa,
Mohammed Bakari ‘Tall’, Abass Dilunga, Aluu Ali, Shabani Baraza na Abdallah
Kibadeni.
Baba yake Saleh
Ruwahi alikuwa ndiye mfadhili wa Simba enzi hizo wakati yeye alikuwa
akivutiwa na wachezaji kama Kibadeni, lakini leo anaendelea kuwa mwanachama wa
Simba na anatoa msaada kwa Messi ambaye ni sawa na mwanaye.
Huenda ukawa ni mfano mzuri wa mwanachama na shabiki wa
Simba wa aina yake aliyeonyesha mapenzi tokea akiwa hajiwezi kifedha hadi leo.
Al Rawahi hakuweza kupatikana na ilielezwa alikuwa
nchini Oman, lakini rafiki yake wa karibu alieleza kwamba kati ya watu Simba
damu, mmoja wapo ni yeye.
“Unajua wakati baba yao alipokuwa mfadhili, walikuwa
wanapelekwa kambini kila siku ya mechi. Wanashinda kule na wachezaji hadi
wakati wa kwenda kwenye mechi.
“Jiulize mtu kama huyo atakuwa na mapenzi na Simba kwa
kiasi gani, maana tokea enzi za Kibadeni wanacheza, yeye alikuwa anakwenda
kambini na baadaye uwanjani.
“Hivyo mapenzi ya Simba si kitu cha kubahatisha kwake.
Na hili suala la Messi kwa kuwa mmelijua, lakini yeye amesaidia wachezaji wengi
sana. Lakini si mtu mwenye majivuno na maneno mengi ndiyo maana amekuwa kimya,”
alieleza rafiki yake huyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment