December 11, 2013





Na Saleh Ally
 UKIFUATILIA kwa umakini uchezaji wa Arsenal, utagundua kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa kiwango hasa katika kiungo.
Hali hiyo imesababisha mashabiki wa Arsenal kusahau kabisa kuhusiana na Cesc Fabregas ambaye waliamini kama angerejea basi tatizo la kiungo lingeisha.
 
Arsenal ina mashabiki wengi duniani kote ikiwemo Tanzania, pamoja na mabadiliko hayo imekuwa ni nadra sana wao kumtaja Aaron Ramsey ambaye ana miaka 22 tu, lakini tayari ameonyesha kuwa ndiye tegemeo la kikosi hicho cha Arsene Wenger.

Raia huyo wa Wales amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu na ndiye anaaminika kuwa kiungo mwenye kiwango cha juu zaidi katika kipindi hiki kwenye Premiership.
Ajabu ni hivi, mashabiki wa Tanzania, England na kote duniani, wamekuwa hawamzungumzii sana na badala yake amekuwa gumzo zaidi kwa wataalamu wa soka.
Gumzo lake kwa wataalamu linatokana na uchezaji wake, hesabu za mambo yake, mabao aliyofunga na pasi alizotoa.


Katika mechi 15 za Ligi Kuu England alizocheza, Ramsey ametoa pasi tano zilizozaa mabao, amepiga mashuti 38 yaliyolenga lango na kivutio zaidi ni mabao nane aliyofunga.

Mabao nane ni katika Premiership, lakini amekuwa pia akifanya vizuri zaidi na kufunga zaidi ya mabao manne kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Ingawa Premiership haijafika hata nusu msimu, tayari Ramsey kitakwimu amefanya kazi mara mbili kuliko ilivyokuwa msimu mzima uliopita.
Wastani wake wa kutoa pasi zilizofika ni 87.2% ambao ni wa juu zaidi na amefanikiwa kuwapiku viungo nyota au walionunuliwa kwa bei mbaya kama Oscar, David Silva, Shinji Kagawa, Marouane Fellaini na hata mkongwe, Mikel Arteta ambaye anapewa sifa ya kumsaidia Ramsey. 

Kwa mguu wa kulia amepiga mashuti kwa wastani wa 82%, kati ya hayo kwa 47%  yalilenga lango na kwa 53%  yalizaa mabao.
Kufanya vizuri kwa Ramsey katika kipindi hiki kunaonyesha uwezo mkubwa wa jicho la Wenger katika vipaji. Wengi wamekuwa wakisahau kazi ya Mfaransa huyo anapokuwa anakuza kipaji.
Lawama nyingi huwa kwake, yakipatikana mafanikio anasahaulika na siku mchezaji akiuzwa lawama nyingi zinaenda kwake.

Aliwahi kutakiwa kuachana na kiungo huyo baada ya Cardiff ambayo alimpeleka kwa mkopo kutaka kumnunua, akakataa. Ikatoa dau ikitaka kumnunua, akakataa pia na baadhi ya viongozi wa klabu wakaona anakosea.
Leo, alichokuwa anakitaka kinaanza kuonekana na aliwahi kueleza kwamba mchezaji mwenye uwezo wa michezo mingine ni rahisi kuwa na mafanikio.
Ramsey alikuwa mchezaji wa mchezo wa raga, maarufu kama rubgy, halafu akashiriki katika riadha za kupeana vijiti katika timu ya shule kabla ya kuamua kujikita kwenye soka.

Kiungo cha Arsenal chenye ‘wabaya’ watatu, Ramsey, Arteta na Mathieu Flamini kimemaliza maisha ya majonzi kwa mashabiki wa Arsenal.
Inawezekana haukuwa ukifuatilia Arsenal inapokuwa inacheza, mechi inayofuata angalia vitu hivi vitatu kutoka kwa Ramsey; kujaribu chochote bila ya woga (anawaudhi mashabiki Arsenal), kuendesha vilivyo kiungo (anamfurahisha zaidi kocha), kutoa pasi au kufunga mabao matata (anarudisha urafiki kwa mashabiki/kocha).

TAKWIMU 2013
MECHI    MABAO    PASI     MASHUTI
    15               8                      5           38



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic