Kocha Mkuu wa Simba, Zdravok Logarusic,
amesema washambuliaji wa timu hiyo, akiwemo Betram Mwombeki, hawajamridhisha na
kuagiza uongozi kumtafutia watu makini zaidi.
Logarusic maarufu kwa jina la Loga,
amesema Mwombeki ni mshambuliaji mzuri wa wastani, ambapo kikubwa ambacho
ameshindwa kukikubali ni jazba zake uwanjani na kutaka uongozi wa Wekundu hao
kusaka mtu makini zaidi atakayesaidiana na Amissi Tambwe.
Loga ambaye ni beki wa zamani wa kushoto
wa Croatia, amesema tayari kazi hiyo ameshawakabidhi viongozi wa Simba, ambapo
amesisitiza kama aina hiyo ya mshambuliaji anayemtaka akipatikana, Wekundu hao
watakuwa na safu kali ya ushambuliaji.
“Nimefanya kazi ya kuwaangalia kwa makini
washambuliaji waliofika mpaka sasa, kidogo huyu Betram (Mwombeki) anaonekana
kuna kitu anacho, lakini tatizo moja alilonalo ni jazba akiwa uwanjani, sijajua
ni mazoezini tu au hata kwenye mechi,” alisema Loga.
“Nimewaambia viongozi kwamba kama
wataweza waniongezee mshambuliaji mmoja mzuri zaidi ya huyu, ambaye
atashirikiana na Amissi (Tambwe), ambaye nimepata sifa zake kwamba ni mtu
makini kwenye kutekeleza majukumu yake ya ufungaji, nataka ubingwa hapa,”
alisema Loga.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment