Na Saleh Ally
Wakati Kocha Alex Chapman Ferguson anastaafu, alizungumzia mambo mawili ambayo aliyaita ni makubwa. Kwanza kuwashukuru kwa miaka takribaki 27 aliyofanya kazi na wakamuunga mkono.
Pili akawaambia kazi kubwa waliyonayo sasa ni kumuunga mkono kocha wao mpya, David Moyes ili kuendeleza mafanikio ya kikosi cha Manchester United.
Inawezekana wanachama na mashabiki wa Man United walimuelewa Ferguson vizuri sana, lakini sasa uzalendo umewashinda na wameanza kumzomea Moyes.
Sababu zaidi ya milioni zinatolewa kuhusu kufanya vibaya kwa Moyes, ilimradi kila mmoja ana zake. Makocha, wachambuzi, watangazaji wa redio, runinga, mashabiki na kila aina ya wadau wa soka wote wana sababu zao.
Kila mmoja anaamini uzito wa sababu zake na kwa upande wa Moyes, mara baada ya vipigo viwili mfululizo ndani ya Old Trafford dhidi ya Everton halafu Newcastle, amekiri kwamba hajawahi kuwa na presha kubwa akiwa kocha kama anayoipata sasa.
Lakini raha zaidi, hata Moyes naye ametoa sababu zake, anakubali kwamba kupoteza pointi 13 kati ya 24 ndani ya Old Trafford si kitu kizuri lakini bado anasisitiza ni kipindi cha mpito.
Hataki kutaja hata siku moja kwamba Ferguson alipotua Old Trafford mwaka 1986 akitokea Aberdeen, alikuwa na kipindi kigumu cha miaka minne hadi mwaka 1990 alipobeba Kombe la FA.
Mashabiki wa Man United walikuwa wakiingia uwanjani na mabango yaliyokuwa yakitaka Ferguson atimuliwe, waliamini timu ya Aberdeen pamoja na kutwaa Kombe la Washindi Ulaya kwa kuifunga Real Madrid, bado ilikuwa ni timu ndogo ukilinganisha na Man United.
Hivyo ni kati ya vitu vinavyomkuta Moyes katika kipindi hiki, mashabiki sasa wamekuwa wakimzomea, wengine wanatoka uwanjani mapema, lakini bado wachache wameendelea kumuunga mkono.
Sababu zinaweza kuwa nyingi sana, tena zinawaudhi mashabiki wa Man United. Mfano Newcastle haikuwahi kuishinda timu yao kwa miaka 41 iliyopita ndani ya Old Trafford, lakini chini ya Moyes hilo limewezekana.
Hofu kubwa kwao ni kukosa hata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitu ambacho Moyes amesisitiza hakitatokea. Tangu ilipoanza kujulikana kama Premier League, Manchester haijawahi kukosa nafasi hiyo.
Pamoja na sababu za kila upande, lakini kuna baadhi ya sababu huenda zikachangia Man United kuendelea kuvurunda kwa kuwa kama ni kikosi kwa asilimia 85 ndiyo kile kilichochukua ubingwa msimu uliopita.
Sababu hizo zinaweza kuchangiwa na Moyes mwenyewe au wanaomzunguka akiwemo Ferguson.
Moja:
Kutoshinda hata kikombe kimoja na kupewa timu kubwa, angalia mambo yalivyokuwa magumu kwa Brendan Rodgers baada ya kutua Liverpool akitokea Swansea. Msimu wa kwanza ulikuwa mgumu sana, lakini sasa ameonyesha njia. Ferguson alipojiunga na Man United, ingawa alitokea timu ndogo ya Aberdeen, lakini ilibeba Kombe la Washindi Ulaya wakati huo na ilianza kuichapa Bayern Munich na baadaye Real Madrid katika fainali.
Mbili:
Linaweza lisionekane ni kosa, lakini kuwepo kwa Ferguson karibu katika kila mechi, huenda kunachangia kumpa Moyes wakati mgumu.
Inaonekana kama Ferguson hajaondoka kwa 100%, huenda itawafanya wachezaji washindwe kumuamini kwa 100% na hisia kwamba hawezi bila ya Ferguson pia ni tatizo na itakuwa rahisi kwao pia kuanza kuchunguza au kujua wapi amepungukiwa kuliko ubora.
Tatu:
Bado imani kwa wachezaji haijawa kubwa, ana kazi kubwa ya kufanya ingawa kwa kuwa amekubali kwenda Man United, hawezi kuwa na muda mrefu unaomsubiri kubadilisha mambo.
Awali ilikuwa rahisi kusikia mchezaji kama Cristiano Ronaldo au wengine kusema anasikia furaha kucheza chini ya Ferguson. Lakini sasa ni vigumu kusikia hata mchezaji mmoja mwenye kiwango cha RVP, mfano Falcao au Lewandowski, akisema anafurahia kucheza chini ya Moyes!
Nne:
Huenda wakati ukazidi kuwa mgumu kwa Moyes hasa kama hatashinda kombe katika msimu huu. Anaweza kuvurugwa zaidi na wachezaji wakongwe ambao wanaamini kuwepo Man United ni kwa ajili ya makombe.
Mfano, Nemanja Vidic, Patrice Evra, Michael Carrick, RVP wanajua umri unawatupa mkono, wanachotaka ni makombe na si hadithi. Ikishindikana, basi watataka kuondoka zao, maana umri hauwasubiri.
Hilo pia ni tatizo na itakuwa moja ya sababu zinazoweza kumuangusha zaidi Moyes ingawa kama ana moyo ‘mgumu’ anaweza kuendelea kubaki na kubadili mambo.
Sababu zinaweza kuwa nyingi zaidi, lakini mwisho ni hivi, ingekuwa maajabu sana kama Moyes angeichukua timu kutoka kwa kocha aliyeifundisha kwa takribani miaka 27 halafu isiyumbe.
Utamaduni wa Man United lazima uko tofauti na timu nyingine yoyote duniani, siyo rahisi kuona inakwenda sawa wakati dereva amebadilishwa tena katika kipindi gari likiwa katika mwendo.
Mwisho wa kila kitu, Man United lazima wakubali kufanya kazi kwa juhudi zaidi kubadili mambo, la sivyo wanaweza kuwa adui wa wao wenyewe kwa kujimaliza wenyewe!
FIN.








mbona huu ndo mwaka wao watajuta sanaaaa.
ReplyDelete