Na Saleh
Ally
AFRIKA
Mashariki na Kati ilishajitoa kabisa katika mbio za kucheza Kombe la Dunia kwa
vile kila inapofanyika michuano hiyo, nchi zinazoshiriki zinatokea Afrika
Magharibi na Kaskazini.
Kanda hizo
mbili za Bara la Afrika ndizo zimekuwa zikitoa washiriki kuiwakilisha Afrika,
angalia hata zilipoongezwa na kufikia timu tano, hakuna timu ya Afrika
Mashariki angalau imepata nafasi ya kutia mguu.
Mwaka 2010
wakati Kombe la Dunia lilipofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, harufu kwamba
angalau nchi za Afrika Mashariki zingeshiriki kwa kuwa ulikuwa wakati mwafaka,
mambo yakawa yaleyale.
Timu kutoka
Afrika Magharibi na Kaskazini ndizo ziliiwakilisha Afrika katika michuano hiyo
iliyomalizika kwa Hispania kubeba kombe kwa kuifunga Uholanzi bao 1-0 kutokana
na shuti la Iniesta.
Nchi
zilizoiwakilisha Afrika zilikuwa ni Ghana, Afrika Kusini, Nigeria, Cameroon, Ivory
Coast na Algeria ambapo Afrika Kusini iliingia kwa kuwa ilikuwa mwenyeji wa
fainali hizo.
Timu tano ndiyo hizohizo zipo tena mwakani
nchini Brazil.
Kuwakilishwa
na timu zilezile katika kipindi cha miaka minane, kunaonyesha hakuna mabadiliko
yoyote ya kisoka kwa Afrika Mashariki.
Achana na
Afrika Mashariki, kikubwa cha kuangalia ni kwamba katika timu hizo za Afrika ni
Ghana pekee ndiyo ilifikia robo fainali mwaka 2010 na nusura ivuke hadi nusu
fainali na kuweka rekodi, lakini mkwaju wa penalti wa Gyan Asamoah ukagonga
mtambaa-panya na kutoka.
Maana yake
hakuna timu ya Afrika imewahi kuvuka robo fainali na kama ni timu zilezile za
2010, ipi ina nafasi ya kupita na kuweka rekodi mpya kwa kuwa inaonekana
zimebanwa?
Cameroon
iko kundi A na Croatia, Mexico na Brazil na inaonekana hapa kazi ya ziada
inabidi ifanyike ili kuvuka hatua hiyo maana Brazil na Mexico ndizo zinapewa
nafasi zaidi wakati Cameroon haina kiwango cha juu sana.
Kundi C
kuna Ivory Coast ambayo itapambana na timu za mabara matatu, Ulaya, Amerika
Kusini na Asia ili ivuke. Bado hakuna timu ya mzaha lakini angalau inapewa
nafasi ya kuzipita Japan, Ugiriki na Colombia na kusonga mbele.
Nigeria
kama itajitutumua, inaweza kusonga kutoka kundi F ambako kuna Argentina,
Bosnia & Herzegovina na Iran. Hata hivyo bado Argentina inapewa nafasi ya
kwanza katika kundi hilo.
Ghana
iliyokuwa inapewa nafasi ya kufanya vyema, iko kwenye kundi G ambalo ni gumu
zaidi kwa timu za Afrika, maana ina Ujerumani, Ureno ya Cristano Ronaldo na
Marekani, maarufu kama wabishi.
Lakini bado
huenda kukawa na matumaini kwa kuwa inaonekana kuwa na kikosi bora ukilinganisha
na timu zote, ingawa ugumu wa kundi ni tatizo.
Timu ya
mwisho ya Afrika ni Algeria ambayo mwaka 2010 pia ilitoka mapema, safari hii
iko kundi H, ambalo lina timu za Ubelgiji, Urusi, Korea Kusini na linaonekana si gumu sana,
hivyo inatakiwa kubadili gia na kuhakikisha inafuzu.
Ukiangalia mpangilio wa makundi na nafasi ya timu za Afrika,
inaonekana kila mmoja anasubiri miujiza kwa kuwa hakuna hata timu moja ya bara
hilo inayopewa angalau kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi.
Timu ya Afrika inayopewa nafasi ya kusonga mbele kutoka
katika hatua ya makundi ni ile inayopewa nafasi ya pili katika kundi.
Hii inaonyesha ni kiasi gani ugumu wa timu za bara hili
kufika mbali katika michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani ingawa katika
mchezo wa soka, mambo yanawezekana kwenda tofauti na yalivyokuwa yanatarajiwa.
Inawezekana
Afrika ikaweka rekodi mpya ya kucheza nusu fainali angalau timu tatu zitavuka
kutoka katika hatua ya makundi na kupambana vilivyo kuifukuzia rekodi hiyo.
Kundi A
Brazil,
Croatia, Mexico na Cameroon
Kundi C
Colombia,
Ugiriki, Japan na Ivory Coast
Kundi
F
Argentina,
Bosnia & Herzegovina, Iran na Nigeria
Kundi
G
Ujerumani,
Ureno, Marekani na Ghana
Kundi
H
Ubelgiji,
Urusi, Korea Kusini na Algeria








0 COMMENTS:
Post a Comment