December 25, 2013




Na Saleh Ally
Kiungo kinda wa Simba, Ramadhani Singano maarufu kama Messi alikuwa kivutio kikubwa katika mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga ambayo inajulikana kwa jina la Nani Mtani Jembe.


Simba walishinda kwa mabao 3-1 huku wakionyesha soka safi, lakini Singano alikuwa kivutio kwa kuwa alicheza vizuri lakini matukio mawili yakakumbukwa zaidi.

Kwanza kumtoka zaidi ya mara moja beki David Luhende hadi akafikia kumkwatua na kusababisha penalti iliyozaa bao la pili, lakini kumpiga chenga ya maudhi Kelvin Yondani iliyosababisha amvute, mwamuzi akampa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu.


Singano ambaye alipewa jina la Messi kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika michuano ya Uhai miaka minne iliyopita, anasema kwamba kila alichokifanya kimetokana na juhudi binafsi lakini pia kuheshimu mawazo ya wanaomzunguka.

“Watu wananipa mawazo, lakini nina kaka yangu ambaye alicheza mpira ingawa hakufika mbali lakini amekuwa ananisaidia sana. Tunaishi naye hapa Keko, ni maarufu sana,” anasema.

Kuhusiana na mechi ya Nani Mtani Jembe, Messi anasema alijua mapema watashinda: “Nilijua Yanga watatudharau, rafiki yangu mmoja nilimuambia tutashinda na Yanga wakitubahatisha, basi sare.”

Wachache:

Siku ya mechi ya Nani Mtani Jembe nilisikia uchungu sana mara baada ya kuingia uwanjani na kuona mashabiki wa Simba walikuwa wachache sana. Ilikuwa ni dalili kwamba mashabiki wa Simba waliingia uoga.

Nawashauri watuamini na wavute subira, waje kwa wingi kutuunga mkono, sisi wachezaji unapoingia uwanjani unakuta mashabiki wachache maana yake hawawaamini si kitu kizuri, waje tu.

Umbo:

Kweli nina umbo dogo, hata mimi wakati mwingine naingia hofu ninapokutana na mabeki wenye maumbo makubwa. Lakini ukubwa wa umbo si kujua mpira, sasa niko tayari kupambana na beki yoyote.

Yondani&Luhende:

Wote ni wachezaji kama mimi, tunapokutana lazima tunashindana. Yondani ni kati ya mabeki bora nchini, hali kadhalika Luhende.

Unapokutana nao lazima utumie ubunifu kuwapita kama ambavyo wao wanafanya jitihada za kunizuia kama mshambuliaji. Hivyo nilijiamini kwamba naweza kupita na nikafanya hivyo kweli.

 Kukatishwa tamaa:

Usipokuwa mvumilivu, mashabiki wengi wanakatisha tamaa kwa kuwa hawapendi mchezaji ashindwe kufunga au akosee. Mpira hauwezi kucheza bila ya kukosea, hilo haliwezekani hata kidogo.

Kuna wachezaji wamekuwa wakikata tamaa baada ya kuandamwa, kweli inauma wakati mwingine kwa kuwa mchezaji anajituma kufanya kitu kizuri lakini inatokea anakosea katika hali ya kawaida ya kimpira. Hivyo mashabiki wajitahidi kuangalia na kukubali kukosea kwa bindamu hata katika maisha ya kawaida kupo na wawaunge mkono wachezaji wao.

Yanga:

Wakati fulani watu waliwahi kuniambia mimi ni Yanga kwa kuwa tu nilikuwa nakosa mabao, hata kidogo sipendi kukosa mabao, lakini inatokea tu mpirani.

Kingine wajue mimi nimekuzwa na Simba, nina mapenzi makubwa sana na timu hiyo. Waliofikiri hivyo waachane na hizo hisia na wakiona nimekosea basi wajue mimi ni binadamu sijakamilika na imenitokea tu.

Milovan:

Milovan (Cirkovic) ndiye kocha aliyeniigiza katika ulimwengu wa soka la kimataifa lakini kabla yeye ndiye aliyeniamini kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nakumbuka ilikuwa ni mechi dhidi ya Azam FC, kweli ilikuwa mechi kubwa sana kwangu lakini akaniambia Messi nakuamini, nenda kacheze na utafanya vizuri. Nilicheza kwa kujiamini ingawa nilikuwa na uoga mwanzo, mwisho tukashinda kwa mabao 3-1.

Baadaye alinipa nafasi kwa mara ya kwanza katika michuano ya kimataifa, tulikuwa Rwanda kucheza dhidi ya Kiyovu, nakumbuka ile mechi ilimalizika kwa sare ya mabao 1-1, nilicheza vizuri pia na kuanzia hapo sina haja ya kuingia hofu.

Makocha:

Sina nia mbaya na makocha wa hapa nyumbani, lengo langu ni kueleza hali halisi kwamba wao wamekuwa hawawaamini wachezaji hasa chipukizi lakini makocha Wazungu wako tofauti.

Akikuona una uwezo, mara moja anakupa nafasi na kukutaka ucheze. Makocha wa nyumbani nao wangejifunza hilo na inawezekana watapatikana wachezaji wengi tu watakaozitumia nafasi na kukua kimchezo.

Kusali&kulala:

Sina mambo mengi sana baada ya soka, zaidi napenda kulala au nitakaa nyumbani na wadogo zangu. Mara nyingi kama utaniona natoka, basi ujue nakwenda msikitini na baada ya hapo narudi nyumbani tena.

Sipendi mambo mengi, nafurahi kuwa na wadogo zangu nyumbani tunapiga stori au kuangalia filamu. Kama si hivyo, nitalala tu.

Bangi:

Kuna watu wamewahi kudhani navuta bangi, sijawahi kufanya hivyo hata mara moja lakini kuna rafiki zangu ambao naamini wanavuta. Lakini sijawahi kuwabagua kwa kuwa kila mmoja ana maisha yake.

Ninaamini hata ukiwa maarufu au una fedha nyingi ni jambo la msingi kuheshimu watu au kuheshimu uhuru wao wa kuchagua wanachotaka katika maisha.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic