Na Saleh Ally
JUZI Jumatatu Mzee Small alizungumzia
kuhusiana na mapenzi yake na mchezo wa soka na namna alivyo na mapenzi makubwa
na Dar Young African maarufu kama Yanga.
Lakini akaeleza namna anavyovutiwa na
uwezo wa mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ambaye ni rafiki
yake.
Pamoja na hivyo, Mzee Small ambaye sasa
ni mgonjwa, anasumbuliwa na ugonjwa wa kupooza upande mmoja aliahidi kuelezea
alivyowahi kukutana na hayati Mwalimu Julius Nyerere na pia rais wa awamu ya
pili, Ali Hassan Mwinyi. Endelea kumfuatilia.
UKIACHANA na soka, Mzee Small ambaye ni
kati ya wasanii wacheshi nchini, anasema alikuwa akikutana na viongozi wengi
wakubwa wa kitaifa kutokana na sanaa hiyo.
Mmoja wa aliokuwa akikutana nao mara kwa
mara na wakati mwingine akawa rafiki yake alikuwa ni Mwalimu Nyerere.
Baba wa Taifa alikuwa akifuatilia
michezo ya Mzee Small na mara kadhaa aliwahi kumueleza anavyovutiwa na umahiri
wake lakini hakuacha kumshauri.
“Nilikutana na Nyerere mara kadhaa, si
kwamba ilikuwa kwa mwaliko maalum lakini alipokwenda kutembelea mabanda kwenye
maonyesha ya Sabasaba alikuwa akiniita.
“Tunakaa hapa na hapa, halafu tunaanza
kuzungumza mambo mengi sana kuhusiana na sanaa ya uigizaji na alikuwa anajua
sana.
“Nilikuwa nasikia faraja sana, unajua
unakutana na kiongozi mkubwa kama yule anakuita jina lako, raha sana. Lakini
anakwenda zaidi ya hapo na kukueleza kwamba alikuwa anafuatilia kazi yako.
“Nyerere alikuwa akinieleza kwamba
anafuatilia sana michezo yangu, tena alionyesha ni mtu anayeijua sanaa kwa kuwa
alikuwa akinikosoa na kunieleza namna mambo yanavyokwenda au anapoamini
nimekosea,” anasema Mzee Small.
Pamoja na Nyerere, Mzee Small anasema
pia amekuwa rafiki wa Rais Mwinyi kutokana na sanaa yake.
“Mwinyi pia ni mtu ambaye alikuwa
akifuatilia kazi zangu, yeye tumekutana mara nyingi zaidi kikazi. Hata sasa
sema ndiyo hivyo kazi na mimi kuumwa zinatutenganisha.
“Lakini kipindi cha uongozi wake
nakumbuka nilipata mafanikio makubwa sana. Kweli ni kati ya watu walionivutia
sana alipokuwa rais,” anasema Mzee Small.
Kuhusiana na heshima ya michezo ya
uigizaji, Mzee Small anasema mambo yamekuwa tofauti kila sanaa hiyo inavyozidi
kupata wigo mkubwa.
“Kila inavyozidi kuendelea na kuwa
kubwa, wasanii wengi wanakuwa hawapendani na ushirikiano si kama ule wakati wa
enzi zetu.
“Kipindi hiki kila msanii anajijali
mwenyewe zaidi, hali hiyo si nzuri kwa sanaa yenyewe. Kila kitu kinatakiwa
kufanyika kwa ushirikiano sana hata kama kila mmoja atakuwa anafanya juhudi
zake binafsi,” anasema Mzee Small.
Kuhusiana na kuendelea na kazi yake,
Mzee Small anasema mara tu atakapopata nafuu, basi atarejea tena na kuendelea
na kutengeneza michezo.
“Sasa kama unavyoona siwezi kitu, lakini
natamani sana lakini uwezo wa kufanya hivyo ndiyo sina. Kama nikipata nafuu na
kupona basi nitarejea tena na kuendelea na kazi yangu,” anasema Mzee Small.
Kawaida analazimika kufanya mazoezi mara
mbili kwa siku ili kuimarisha viungo vyake hasa ule upande uliopooza na kwa
kiasi kikubwa mazoezi hayo yanamsaidia kupata nafuu.
MWISHO
YA SIMULIZI ZA MAISHA YA MZEE SMALL KWA UFUPI. KWA WALE WENYE UWEZO WA
KUMSAIDIA MATIBABU KWA KUWA SASA HANA KIPATO, WANAWEZA KUFANYA HIVYO.
0 COMMENTS:
Post a Comment