Mtoto wa kwanza wa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amelazwa mahututi katika hospitali iliyoelezwa
kuwa katika Mji wa Atlanta nchini Marekani.
Taarifa za kulazwa kwa mtoto huyo wa kwanza wa Rage ambaye jina lake
halikupatikana mara moja zilianza kuenea juzi na baadaye jana, ambapo watoa
habari walieleza kwamba mtoto huyo wa Rage amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi
(ICU) baada ya kugundulika mwilini mwake kulikuwa na sumu.
“Tumesikia kuwa mtoto wa mwenyekiti amenyweshwa sumu, lakini tumekuwa
hatuna uhakika kwa kuwa taarifa tuliyoipata klabuni imeeleza kwamba mtoto wake
yuko ICU ingawa hatujui ukweli wa mambo,” alisema mmoja wa wanachama wa Simba.
Taarifa hizo zilienea haraka jana na juhudi za Championi Ijumaa kupata
uhakika wa jambo hilo ziliyumba baada ya kila aliyeulizwa wakiwemo viongozi wa
Simba kusema pia walikuwa wakilisikia juujuu.
Lakini mmoja wa viongozi wa Simba alisema: “Ukweli ni hivi, mwenyekiti
amewatumia email baadhi ya viongozi na kusema mtoto wake huyo yupo ICU, lakini
sasa hakuna mwenye uhakika kama ni sumu ingawa wote tumesikia kwamba mwanaye
kanyweshwa sumu.”
Baada ya hapo gazeti hili zikafanyika juhudi kumpata mkewe ambaye yuko
jijini Dar es Salaam, simu ilipokelewa na kitinda mimba wa Rage ambaye alisema
mama yake ameiacha simu hiyo.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, kidogo alionekana kujichanganya
ingawa alikiri kuwa kweli kaka yake alikuwa amelazwa nchini Marekani katika
chumba hicho cha wagonjwa mahututi.
“Kweli alikuwa amelazwa, lakini leo ametoka na anaendelea vizuri,”
alisema na alipoulizwa kuwa kama sumu ilihusika, alijibu:
“Anaumwa pneumonia (rimonia) tu, ingawa sumu imeisha mwilini.”
Alipotakiwa kufafanua kuhusiana na sumu iliyoisha mwilini, akaongeza: “Mama
akija anaweza kuzungumzia hili.”
Taarifa nyingine zimeeleza kuwa suala hilo limekuwa likifanywa siri kubwa
na familia ya Rage ndiyo maana imekuwa vigumu kuliweka wazi.
Rage ana watoto wanne, wa kwanza ni huyo ambaye ni mgonjwa na amekuwa
akiishi nchini Marekani wakati wa pili ni wa kike ambaye anaishi nchini
Australia. Mtoto wake wa tatu pia anasoma chuo mwaka wa kwanza huko Australia.
Aliyezungumza na Championi Ijumaa ni mwanaye wa mwisho ambaye anasoma
sekondari moja maarufu hapa jijini Dar.
POLE:
Kwa niaba ya timu nzima ya Championi, tunamuombea Rage apate ujasiri na
nguvu ili apambane katika wakati huu mgumu na kulimaliza tatizo hilo, pia Mungu
amsaidie mwanaye kupata nafuu, apone kabisa.
MHARIRI KIONGOZI.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment