Yanga ndiyo
mabingwa Tanzania Bara, Yanga ndiyo klabu na timu maarufu kwa maana ya kuungwa
mkono na mashabiki wengi zaidi.
Kumekuwa na
ubishi kuhusiana na hilo, kwamba timu ipi kati ya Yanga na Simba ina mashabiki
wengi kuliko nyingine lakini inaonekana hakuna uchunguzi wa kutosha
kuthibitisha hilo.
Lakini kwa
mechi za Ligi Kuu Bara kwa maana ya mashabiki walioingia kwa wingi uwanjani kwa
upande wa Simba na Yanga, utagundua wengi zaidi walikuwa wa Jangwani na hata
kwa mapato kwa mzunguko wa kwanza, Yanga imeshika nafasi ya kwanza na kufuatiwa
na watani wake ingawa si kwa tofauti kubwa sana.
Nani ana
mashabiki wengi zaidi si hoja ya msingi leo, lakini taarifa ya mapato na
matumizi ya Yanga iliyotolewa siku chache zilizopita kiasi fulani inatia hofu
mwenendo wa soka nchini.
Katika
taarifa hiyo ya mapato iliyoanzia Januari 15 hadi Aprili 14, mwaka huu na
Aprili 15 hadi Julai 14, 2013, Yanga imekuwa ikijiendesha kwa hasara.
Katika
kipindi cha kwanza, Yanga ilipata hasara ya Sh milioni 99.5 na kipindi cha pili
kilichoanzia Aprili 15, Yanga ikaingia hasara tena ya Sh milioni 55.4.
Kwa
kuangalia kawaida, inaonekana ni kitu cha kawaida kabisa na inajulikana katika
biashara kuna faida na hasara, kikubwa ni kujipanga na kufanya mambo yaende
vizuri.
Lakini kama
utajiuliza, inafikia Yanga, klabu kubwa, yenye mashabiki wengi vipi
inajiendesha kwa hasara? Kama kweli vigezo vya kuiendesha klabu ikiwa haina
shida kifedha ni mashabiki, wadhamini na haki za runinga, vipi Yanga inapata
hasara?
Ukiangalia
vitu viwili vya mwanzo yaani mashabiki na wadhamini, tayari Yanga inao na
kinachotakiwa ni kuongeza ubunifu zaidi ili kuwapata wengi zaidi. Lile la tatu,
bado limekuwa na mvutano kati ya Yanga na Azam TV, huenda likapata jibu hapo baadaye.
Lakini
wakati Yanga inaendelea kusubiri kuhusiana na suala la Azam TV, bado ina nafasi
ya kujiendesha kwa faida kwa kuwa ina kila sababu ya kufanya hivyo.
Jiulize
kama Yanga itakuwa inajiendesha kwa hasara, vipi kwa timu nyingine ambazo
haziwezi kufikia hata robo ya mashabiki wa klabu hiyo?
Uongozi wa
Yanga unaweza kulalamika, mfano una sababu kadhaa ambazo ni za msingi kweli
hasa kuhusiana na kupungua kwa mashabiki uwanjani. Lakini bado kuna mambo mengi
ya kufanya na kuendesha klabu hiyo kwa mwendo wa biashara zaidi.
Mfano, ni kuzitangaza
mechi ikiwa ni pamoja na kuweka vivutio fulani ili kuvutia watu wengi zaidi
kwenda uwanjani. Kushauriana na TFF katika suala la kupanga ratiba na kuwaeleza
kuangalia suala la mapato badala ya kupanga ratiba inayolenga kumaliza ligi tu.
Lakini
wanaweza kutanuka kibiashara zaidi kama vile kusimamia vilivyo mauzo ya jezi
zao ili fedha iingie klabuni, kuwa na kitengo cha masoko kitakachofanya mambo
kwa utaalamu na kuangalia kama Yanga inaweza kuuza fulana zenye picha za
wachezaji, jezi zikiwemo zenye majina ya wachezaji maarufu zaidi.
Yanga
inaweza ikaingiza kipato kikubwa hata kabla ya viingilio vya uwanjani au fedha
za runinga. Lakini inaonekana kila kitu kinakwenda kwa kufuata mazoea, kitu
ambacho si sahihi pia ni tatizo.
Yanga iko
kwenye bahari ya utajiri, kinachotakiwa ni ubunifu. Hivyo uongozi wa Yanga
unatakiwa kubadilisha mambo ili kwenda kisasa na kitaalamu zaidi ili kuondokana
na maisha ya enzi zile yalizozidumaza klabu hizo maarufu ambazo majina yake
yamebaki kuendelea makubwa, lakini hazina kitu.
0 COMMENTS:
Post a Comment