Na
Saleh Ally
MCHEZAJI
nyota wa zamani wa Manchester United, Bryan Robson amewafungua macho wapenda
soka kwamba wanaweza wakafanya mambo mengi makubwa wakiwa hapa nyumbani na
hakuna haja ya kutegemea msaada.
Robson
ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya England amepanda Mlima
Kilimanjaro pamoja na mchezaji mwingine wa zamani, Kevin Moran ambaye pia
alikipiga Man United, enzi zake.
Robson
mwenye miaka 56, amepanda mlima huo na kufanikisha kuchangisha pauni 115,000
(Sh milioni 287.5) kwa ajili ya kuwachangia wanaosumbuliwa na kansa ya koo.
Staa huyo alifanya tukio hilo miezi michache baada ya kupona kansa ya koo.
Safari
yake ya siku tano kupanda mlima huo inavutia na katika mahojiano na Gazeti la Dailymail,
Robson aliyewahi kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Championi anaeleza namna
walivyoanza baada ya kuwasili nchini hadi walivyofika kileleni.
Kilimanjaro
ndiyo mlima mrefu kuliko yote barani Afrika, wakati fulani Wakenya walikuwa
wakiutumia kujifaidisha huku wakiwadanganya watu kwamba uko nchini mwao.
Inaonekana
sasa Watanzania wameamka na kulizuia hilo ndiyo maana utaona nyota wengi
duniani wamekuwa wakija nchini na kuupanda.
Lakini
wakati Robson na wenzake wakipanda na kufanikiwa kuchangisha mamilioni ya fedha
kwa ajili ya kusaidia wenye matatizo ya kansa ya koo, wanamichezo wa Tanzania
bado wamelala usingizi.
Ingawa imekuwa kipindi kidogo tokea afanye hivyo lakini
nyota huyo wa Manchester United hata kama atakuwa ametumiwa na kampuni fulani
pamoja na mwenzake Moran wameona kupitia Mlima Kilimanjaro wanaweza kufanya
kitu fulani kusaidia.
Kweli wameingiza mamilioni ya fedha kusaidia huku kampuni
kibao na idara nyingi zikiwemo taasisi na mashirikisho ya michezo yakiwa
hayajui umuhimu wa mlima huo.
Michezo ina nguvu ya kusaidia na kuongoza mambo mengi
kwenye jamii lakini wanaoiongoza hawalijui hilo ndiyo maana wamelala.
Inawezekana pia kwa kuwa kumekuwa na mashindano ya riadha,
basi huenda wengi wanaona mchezo unaoweza kuhusishwa na mlima huo ni riadha
pekee, kitu ambacho si sahihi.
Kwa wale wanaofuatilia Ligi Kuu England, wakiwa makini
wataona lile tangazo la Adidas linalomhusisha mshambuliaji nyota wa Barcelona,
Lionel Messi akiwa kwenye kilele cha mlima huo ulio Kaskazini mwa nchi yetu.
Mlima Kilimanjaro ingawa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, Watanzania hata hawajui cha kuufanyia na badala yake wajanja kutoka nje
kama ilivyokuwa kwa Wakenya, wamekuwa wakiutumia kujifaidisha wao binafsi na
watu wa nchi zao.
Wakati wa kutoa tongotongo umefika, Watanzania ambao
wanaweza kufanya jambo na sasa kupitia michezo basi wanaweza kufanya hivyo ili
kuisaidia jamii ya nchi yetu.
Robson amechangisha kwa ajili ya wanaosumbuliwa na kansa
ya koo, lakini kuna wengi wanaweza kusaidia, hivyo tujifunze ingawa limekuja
kufanyika kwetu basi si vibaya kujua njia za kupita na mlima huo utumike
kupitia michezo.
Kwa kuitumia michezo, kupitia Mlima Kilimanjaro kunaweza
kuwa na misaada mingi na wanamichezo wawe tayari kujitolea kwa ajili ya jamii yao,
si kila kitu lazima faida iwe kwao.
Siku tano za Robson kufika kileleni anaeleza mambo mengi
ikiwa ni pamoja na kuteseka na baridi kali, kulala kwenye mahema lakini mwisho
amefanikiwa kufikia malengo yake. Wanamichezo wa Tanzania wenye nia na upendo na
nchi yetu, wanaliweza hili.
Lakini lazima wakubali kuanza na nia, waende kwenye
ubunifu lakini muhimu ni kutaka kutekeleza jambo na mwisho, kuumia kwa ajili ya
watu wako, yaani jamii iliyokuzunguka, jamani Mlima Kilimanjaro ni neema.
0 COMMENTS:
Post a Comment