Hali si shwari kwa baadhi ya
wachezaji wa Yanga baada ya juzi Jumamosi uongozi wa timu hiyo kuwapa barua za
onyo kuhusu utovu wao wa nidhamu na mambo mengine klabuni hapo.
Imeelezwa kuwa, juzi kiungo wa timu
hiyo, Athumani Idd ‘Chuji’, alipewa barua ya kusimamishwa klabuni hapo kwa siku
zisizojulikana huku nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haruna Niyonzima, raia wa
Rwanda, Jerry Tegete na David Luhende wakipewa za onyo kali.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga umekuwa
na siri kubwa kueleza ni utovu gani wa nidhamu uliosababisha Chuji
akasimamishwa na wengine kupewa onyo kali.
Chuji alikasirika baada ya kutolewa
uwanjani mara baada ya kumalizika kipindi cha kwanza cha mchezo wa Nani Mtani
Jembe na kuondoka moja kwa moja kwenda nyumbani hali ambayo viongozi wameona ni
dharau.
Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga
kimeliambia gazeti hili kuwa, viongozi wa ngazi za juu Yanga walikutana Ijumaa
iliyopita, kujadili masuala mbalimbali ya klabu lakini kubwa lilikuwa juu ya
wachezaji hao.
Kilisema kuwa kila mchezaji
alijadiliwa kulingana na maisha anayoishi klabuni hapo pamoja na nidhamu yake
kiujumla ambapo walikubaliana kumsimamisha Chuji, kisha wengine kupewa onyo
kwanza kabla ya kuchukua hatua nyingine kubwa zaidi.
“Mipango ilikuwa ni kuangalia tatizo
liko wapi Yanga, mara baada ya benchi la ufundi kusafishwa, lengo likawa kurudi
kwa wachezaji ambapo tayari Chuji ameshasimamishwa na wengine wamepewa barua za
onyo kali.
“Tegete, Niyonzima, Cannavaro na
Luhende ndiyo wamepewa hizo barua, wameambiwa wajirekebishe mienendo yao wakiwa
Yanga,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Lakini wachezaji wote walikana
kuhusiana na suala hilo na kwamba hawajapokea barua yoyote.
“Mi sijapokea barua ya onyo lolote,
huo ni uongo, kama ningepewa ningekwambia.”
0 COMMENTS:
Post a Comment