Sakata la mshambuliaji wa Yanga SC, Emmanuel
Okwi kuzuiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuichezea klabu hiyo,
limeifanya Yanga kuweka kando kwa sasa suala la kiungo wake Athumani Idd
‘Chuji’.
Okwi alisimamishwa na shirikisho hilo
siku mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kwa madai ya kutaka
kujiridhisha na usajili wa raia huyo wa Uganda kutoka Klabu ya Villa ya Uganda
huku akiwa na mgogoro na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Yanga sasa imekuwa ‘bize’ kuhakikisha
inalitatua suala hilo mapema haraka iwezekanavyo huku majadiliano juu ya
msamaha wa Chuji yakiendelea kusubiri pembeni.
Katibu
Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alisema bado hajajua kinachoendelea kuhusu Chuji kwa
kuwa kuna vitu vingi vilijitokeza hapa kati na vinahitaji kuwekwa sawa haraka iwezekanavyo,
likiwemo suala la Okwi.
Alisema sakata la Okwi ambaye ni
mchezaji wa zamani wa Simba, lilikuja ghafla mezani kwake hivyo kutokana na
majukumu hayo, mpaka sasa hajapokea taarifa ya kinachoendelea kwa Chuji
kutokana na kuwa na kazi hiyo nyingine inayohitaji utatuzi wa haraka.
Alifafanua kuwa, kuna kamati maalum
inayolishughulikia sakata la kiungo huyo ambayo mpaka sasa bado haijampa
taarifa ya kinachoendelea juu ya hayo yote ambapo inaonekana dhahiri kuwa
likimalizika la Okwi ndiyo la Chuji litajadiliwa.
“Hapa kati kulikuwa na muingiliano wa vitu
vingi vilivyohitaji kushughulikiwa kwa haraka zaidi, kulikuwa na maandalizi ya
ligi, suala la Okwi kwa hiyo mezani kwangu hayo yakawa yamechukua hatamu kwa
kuwa yalihitaji uharaka zaidi.
“Ila kuhusu suala la Chuji bado lipo
ingawa kuna kamati inayolishughulikia hili ambayo bado haijanijuza nini
kinaendelea na sijajua kama inaweza kukaa tena lini kujadiliana lakini kwa sasa
kubwa nililonalo ni hili la Okwi,” alisema Njovu.
0 COMMENTS:
Post a Comment