Pamoja na taarifa za
awali kueleza beki Shomari Kapombe amerejea Ufaransa kuungana na timu yake ya
AS Cannes, taarifa za uhakika zinaeleza bado amekwama nchini na amejichimbia
kwao mkoani Morogoro.
Kapombe ameendelea kuwepo
nchini tangu Desemba, mwaka jana aliporejea kuitumikia timu ya taifa, katika
mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe, ambapo inaelezwa kutokana na safari yake
kutoeleweka, amekuwa hapendi kuonekana hadharani kukwepa maswali.
Mtu wa karibu wa mchezaji
huyo ameliambia gazeti hili kuwa, kuna vitu havijakamilika ndiyo maana
ameshindwa kuondoka.
Awali, Shirikisho la Soka
la Tanzania (TFF) lilihojiwa na gazeti hili na kusema lilimsaidia kukamilisha
kila kitu kwa ajili ya safari yake.
“Sasa hivi itakuwa zaidi
ya miezi miwili, kuna masuala yake yamemkwamisha, mara nyingi anakuwa kwao
Morogoro lakini muda wowote ataondoka,” alisema mtu huyo.
Championi Ijumaa
lilimpigia Kapombe simu kupitia namba yake ya Tanzania, ambapo alipokea na
kusema: “Nitakupigia baadaye.” Kisha akakata, alipopigiwa baadaye, simu iliita
bila kupokelewa.
Alipoulizwa Ofisa Habari
wa TFF, Boniface Wambura, alisema: “Sisi tulimkamilishia kila kitu, hivyo kama
amekwama au la, hilo sisi hatujui.”
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment