Kocha Mkuu wa Ashanti United, Abdallah
Kibadeni, amesema atahakikisha anaifunga Yanga kwenye mechi ya kwanza ya Ligi
Kuu ya Tanzania Bara mzuguko wa pili Jumamosi.
Yanga ipo Uturuki kwa takribani wiki
mbili sasa kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi na michuano ya
Klabu Bingwa Afrika ambapo inatarajia kurejea nchini kesho Alhamisi, lakini
Kibadeni, kocha wa zamani wa Simba, amesema hata iweje watawazima tu.
Kibadeni alisema kuwa hawezi kuihofia
Yanga kwa kuwa imeenda kujiandaa Uturuki ambapo anaamini kuwa maandalizi ni
mahali popote pale na wala hawawezi kufungwa kirahisi kwa kuwa wao Ashanti
waliweka kambi Bamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.
“Nia yetu ni kuibuka na ushindi na wala
si kingine, japokuwa inategemea mtu utacheza vipi siku hiyo, lakini hatutakuwa
na hofu kwamba tunacheza na Yanga ya Uturuki, hatuwezi kuhofia hilo, maandalizi
ni popote tu, wao wapo Uturuki sisi tupo Bamba, lakini mechi ndiyo itaamua nani
alijiandaa vizuri,” alisema Kibadeni.
Kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa
ligi, Yanga iliyokuwa chini ya Mholanzi, Ernie Brandts, iliifumua Ashanti
iliyokuwa chini ya Hassan Banyai mabao 5-1.
0 COMMENTS:
Post a Comment