Kitendo cha
Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic kumwingiza na kumtoa mshambuliaji wake
Betram Mwombeki ndani ya dakika chache, kimewakera watu wengi na Mwenyekiti wa
Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoki amefunguka na
kusema haikuwa sahihi.
Kisoki ambaye ni bosi wa wachezaji wote wa Ligi Kuu
Bara, amesema yeye binafsi ameshangazwa na kitu hicho na kushauri uongozi wa
Simba ulifanyie kazi suala hilo na ikiwezekana umpe onyo Logarusic.
“Sitaki
kuingilia uamuzi wa kocha, wala sitaki kusema hajui kazi yake. Lakini alichokifanya
kwa Mwombeki si sahihi na kinaweza kummaliza mchezaji. Kocha lazima aangalie
kwamba kama kweli mchezaji anataka kumtumia siku nyingine, basi asimfanyie
vitendo vinavyoweza kumuathiri.
“Nilihesabu
baada ya Mwombeki kuingia alicheza mipira mitano, alikosea miwili, mitatu akatoa
pasi ukiwemo mmoja ambao alimpa pasi (Ramadhani Singano) Messi na angeweza
kufunga lakini akashindwa. Sasa hilo ni tatizo la kumtoa mchezaji! Hata kama
mimi si kocha lakini si sahihi.
“Inawezekana
watu wakalizungumza hili suala kishabiki, lakini haya ni mawazo yangu na kwa
kuwa ni mmoja kati ya wanaosimamia haki za wachezaji, naomba niseme wazi kuwa
halikunifurahisha hata kidogo.
“Mpira ni
mchezo wa makosa, kama mtu akikosea mara mbili anatolewa, basi Kiemba, Chanongo
wote wangetolewa. Ingawa bado nasisitiza hiyo si sahihi,” alisema Kisoki ambaye
pia ni mdau mkubwa wa soka.
“Ingekuwa
Ulaya, vyama vyao vina sauti tofauti na hapa. Maana hata kuna mashabiki wanaona
mchezaji ana makosa, lakini si sahihi, hata kupasha mwili inahitaji muda na
lazima ujue Mwombeki ana umbo kubwa.
“Makosa
kila mtu anayo, angalia hata kocha alikosea. Mchezaji anapiga penalti yeye
anaangalia majukwaa, hilo ni kosa, lakini ndiyo kuvumiliana maana hata kama ni
mchezo kuna ubinadamu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment