Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi,
amesema kuna ulazima ratiba ya Ligi Kuu Bara kurekebishwa kwa sababu mapumziko
ya muda mrefu yanawaathiri sana wachezaji na kurudisha nyuma kiwango cha soka.
Mbeya City ilishindwa kutamba
katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini ikikomaa kwenye mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu Bara kwa kuwahenyesha vigogo na kushinda nafasi ya tatu, ikiwa nyuma
kwa pointi moja tu dhidi ya vinara, Yanga.
Mwambusi alisema mapumziko ya muda mrefu yanaathiri sana viwango vya wachezaji, japo Kombe la Mapinduzi liliwasaidia kugundua
matatizo yao kiufundi.
Mwambusi alisema kwa sasa anaendelea
kuwaandaa wachezaji wake ili kuweza kuhakikisha wanafanya vyema katika mzunguko
wa pili unaotarajiwa kuanza Jumamosi wiki hii.
“Maandalizi yanakwenda vizuri lakini
mapumziko ya muda mrefu yamewaathiri sana wachezaji wangu, kama kuna uwezekano
wa ratiba kubadilishwa ni bora ikawa hivyo kuliko kuchukua muda, viwango na
uwezo wao unapotea lakini nashukuru hili nimeligundua mapema kupitia Mapinduzi.
“Tumebakiza siku chache sana kabla ya
ligi kuanza lakini sisi matumaini yetu ni kuanza vyema na kuendelea kuutafuta
ubingwa,” alisema Mwambusi.
Mbeya City itafungua pazia lake la
mzunguko wa pili kwa kuvaana na Kagera Sugar ugenini kwenye Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba.
0 COMMENTS:
Post a Comment