Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi amesema hataki kuzisikia wala kuzungumzia habari
za Simba na Etoile du Sahel kwa kuwa hana mpango wa kurejea alikotoka.
Okwi
ametoa tamko hilo ikiwa ni siku chache mara baada ya kupewa ‘kifungo’ cha muda,
huku uongozi wa Yanga ukisisitiza kuwa utamtumia mchezaji huyo katika mechi ya
Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Komorozine ya Comoro inayotarajiwa kuchezwa
wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Okwi ambaye ni raia wa Uganda, alisema yeye ni mchezaji wa
Yanga na mapenzi yake yapo klabuni hapo, ndiyo maana hataki kuzungumzia suala
la mgogoro wa usajili wake, kwa kuwa hana mpango wa kurudi alipotoka.
“Najua
baada ya muda TFF itaniruhusu kucheza, sitaki kurudi nilipotoka kwa
kulizungumzia suala la Etoile (du Sahel), pia sitaki kuizungumzia Simba kwa
kuwa siyo klabu yangu.
“Naipenda
Yanga na mapenzi yangu yote yapo hapa, ndiyo maana leo hii nipo klabuni nikiwa
mchezaji wao. Nilikuwa tayari kuanza kuichezea Yanga katika ligi hii (mzunguko
wa pili wa Ligi Kuu Bara) na Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Okwi.
Akizungumzia
juu ya sakata la kuzuiwa kwa Okwi, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu ameliambia
gazeti hili kuwa, watamtumia Okwi katika mechi dhidi ya Komorozine kwa kuwa wamepata ruhusa ya kumtumia
kutoka Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).
“Caf
wametupa ruhusa ya kumtumia, sisi tunawaamini wao, kwani inavyoonekana TFF
ndiyo hawamtaki (Okwi) kwenye ligi yao, sisi tunajua Caf ni wakubwa kuliko TFF,
hivyo tutamtumia siku hiyo.
“TFF
hawakutupa muda wa kujitetea walipomsimamisha Okwi, tulianza kuona taarifa hizo
kwenye vyombo vya habari, baadaye ndiyo wakatupa barua, kwa hiyo Okwi tutaanza
kumtumia rasmi kwenye mechi dhidi ya Komorozine,” alisisitiza Beno.
Wakati
huohuo, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema anaamini tayari Fifa
watakuwa wameshateua jaji wa kusikiliza kesi ya mchezaji huyo.
“Hatuna
shida ya kuwaandikia barua ya kuwauliza Fifa kile kinachoendelea, tarehe ya
awali iliyowekwa ni Januari 27, mwaka huu waliyotakiwa kuwa wametulipa fedha za
usajili lakini hawajafanya hivyo,” alisema Kamwaga.
0 COMMENTS:
Post a Comment