Na Mwandishi Wetu
MAMBO yamekucha kwa kiungo nyota wa Simba, Ramadhani
Singano ‘Messi’ baada ya klabu tajiri ya TP Mazembe ya Lubumbashi, DR Congo
kuonyesha wazi kuwa inamtaka.
TP Mazembe tayari imetuma mtu ambaye amekuja nchini
kwa ajili ya kumshuhudia Messi akiichezea Simba na ameeleza nia ya klabu hiyo.
Shushu huyo wa usajili wa TP Mazembe alikuwa uwanjani
wakati Simba ikicheza na Rhino ya Tabora kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumapili
na kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Messi.
Habari za uhakika zimeeleza mara baada ya mtu huyo
kumshuhudia Messi akifunga bao na pia kukosa penalti amewaeleza viongozi wa
Simba kutokana na nia ya klabu hiyo maarufu barani Afrika.
“Jambo hili bado ni siri kubwa, lakini TP Mazembe
walimtuma mtu wao, huyo ndiye alitumwa mara ya kwanza kuifanyia umafia Simba
kabla ya TP Mazembe kuja hapa kucheza.
“Alipokuja akamuona (Mbwana) Samatta na kuwaambia kuna
mchezaji hatari, ndiyo maana uongozi wote wa juu wa TP Mazembe ukaja kuja
kushuhudia mechi hiyo na kweli Samatta akafanya vizuri.
“Kutokana na hali hiyo huyo jamaa anaaminiwa sana,
akirudi na kusema Messi yuko safi, basi jamaa watakuja kufanya rasmi mazungumzo
na Simba,” kilieleza chanzo cha uhakika.
TP Mazembe sasa inamlipa Samatta kitita cha dola
10,000 (Sh milioni 16.5), kwa mwezi. Kama itafanikiwa kumpata Messi, basi
huenda akachota kuanzia dola 3,000 hadi 5,000, kwa mwezi.
Messi amekuwa gumzo kuanzia mwanzo wa msimu huu kutokana
na kiwango chake kupanda kwa kasi kubwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment