Na Saleh Ally
HAKUNA anayeweza kupinga kwa kipindi hiki kwamba
mchezaji kinda wa kikosi cha Simba, Ramadhani Singano, ndiye kiungo wa pembeni
tishio zaidi hasa kama utachukua katika kundi la wanaochipukia kwa kasi.
Singano ambaye jina lake la utani ni Messi, pia
anaingia hadi katika kundi la wakongwe na wengi wameanza hata kulinganisha
uwezo wake na nyota wengine kama Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na wengine ambao
wanajulikana kuwa uwezo wao uko juu.
Kiungo huyo mwenye kasi amekuwa tishio kwa mabeki wote
wanaokutana na Simba na wamekuwa wakimzungumzia kwamba kweli ‘anatisha’
kutokana na uwezo mkubwa alionao, hilo halina ubishi na uwezo wake uko wazi.
Kadiri siku zinavyosonga mbele, gumzo la Messi
linazidi kupanda, Singano anakuwa Messi wa kwanza kupanda na kupata mafanikio
ukilinganisha na wengine kwa kuwa jina hilo la mshambuliaji nyota wa Argentina,
Lionel Messi, wamebandikwa wachezaji wengi sana.
Katika kina Messi, Singano ndiye ameanza kuonyesha
kweli waliompa jina hilo waliona mbali kwa kuwa uwezo wake sasa uko juu, pia ni
gumzo. Kwani katika umri wa miaka 22, tayari amekuwa tegemeo la kikosi cha timu
kubwa kama Simba.
Hivi karibuni, gazeti hili liliandika makala nzuri
kuhusiana na Messi, maisha yake na hadi mwanachama mmoja wa Simba, Musley Al
Rawahi, aliyeamua kujitolea na kumnunulia gari kinda huyo ikiwa ni kama sehemu
ya motisha kwake ili aweze kujituma zaidi kwa mafanikio yake na Simba pia.
Uamuzi wa Al Rawahi, unaweza kufanywa na wanachama au
mashabiki wachache sana wa soka, wengine wanaweza wakashindwa kutokana na
kutokuwa na uwezo wa kifedha, lakini wengine wanaweza kuwa na uwezo huo lakini
wasiwe na moyo tu wa kujitolea, yote yanawezekana.
Inawezekana motisha ambayo aliitoa Al Rawahi kwa Messi
inaweza kuwa ilichangia kwa kiasi kikubwa yeye kuamka na kuongeza juhudi,
lakini bado kwa umri alionao, kuna mambo mawili makubwa yanatakiwa kufanyika. Kwanza
kwake mwenyewe na pili kwa jamii nzima inayomzunguka na hasa watu wa karibu
yake.
Tukianza naye, Messi anaonekana si mtu wa mambo mengi
na maisha yake hayana makuu. Anapenda kushinda nyumbani, kukaa karibu na
familia yake na si mchezaji anayetaka kuonekana akiwa sehemu mbalimbali akinywa
vileo au makundi ambayo unaweza kuyaita si mazuri.
Kwake kazi ya kuendelea kufanya vizuri kwa muda mrefu,
inaweza kuwa rahisi kwa kuwa njia anayopita hadi sasa ni nzuri. Kikubwa
anapaswa kuidumisha na kuamini mafanikio anayopata sasa ni kiduchu tu, anaweza
kupata zaidi ya hapa tena kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na kwamba anaonekana anakwenda kwa mwenendo
mazuri, lakini Messi ni binadamu kama wengine, hakuna aliyekamilika, hivyo
anaweza kufanya lolote ambalo ni tofauti na matarajio ya wengi na mwisho
akaangukia kwenye njia ya kufeli.
Kila binadamu anayefeli anaye wa kumsingizia, si mwingine
zaidi ya shetani. Lakini ukweli mara nyingi anayefeli chanzo huwa ni yeye
mwenyewe, Messi anaweza kulikataa hilo na mwisho mafanikio yakasonga mbele zaidi.
Kwa kuwa sasa anamiliki gari moja, basi ana uwezo wa kumiliki zaidi ya kumi,
nyumba na vinginevyo kupitia mpira huohuo.
Jambo la pili, jamii inayomzunguka. Hii ina kazi kubwa
sana kuhakikisha Messi hakwami mapema kama ambavyo tumeona kwa wengine wengi
walioibuka na kufanya vizuri kwa kasi kubwa, halafu wakaporomoka kama gunia
lililokuwa limefungwa kamba linapandishwa juu ya gari, halafu ghafla kamba hiyo
ikakatika.
Mwenyewe Messi aliliambia gazeti hili kwamba kuna kaka
yake amekuwa akimshauri vizuri sana, huyo anaweza kuwa mtu muhimu kwake.
Watakuwepo watu wengine ambao wanataka mafanikio yake pia, lakini bado kutakuwa
na kundi lenye nia moja tu, kumjaza sifa ili kujifurahisha nafsi zao, sawa na
mashabiki wa Simba wanaotaka kuwakoga wenzao wa Yanga.
Sifa hazitaisha, hata kwenye vyombo vya habari
vitakuwepo, lakini kama mchezaji atafeli eti kwa kuwa alisifiwa kwenye vyombo
vya habari, basi hilo ni tatizo lake na unaweza kusema si mchezaji makini na
hakuwa anajitambua.
Mafanikio ya mtu, yanaendana na pongezi na sifa,
lakini kujitambua ni muhimu zaidi. Kama vyombo vya habari vingekuwa
vinasababisha mtu afeli kwa kumsifia tu, basi leo Cristiano Ronaldo, Wayne
Rooney, Lionel Messi na wengine wengi wasingekuwepo kabisa. Lakini kila mmoja
afanye kazi yake na ajitambue, hakuna atakayefeli.
Hivyo jamii inayomzunguka Messi, inapaswa imkumbushe,
kwamba alipofikia bado lakini anajitahidi na anachotakiwa kufanya ni kuongeza
juhudi zaidi ili afanikiwe zaidi kwa kuwa kipaji alichobarikiwa na Mwenyezi
Mungu ni zawadi kubwa inayoweza kumsaidia kuishi maisha bora maradufu ya sasa
kutokana na mafanikio atakayoyapata.
Mafanikio yanahitaji juhudi na maarifa lakini lazima
kuwe na subira ya muda, kwamba kila unachokifanya ili kufanikiwa, matokeo huja
baada ya muda fulani, usipokuwa na subira, basi hutafikia malengo ya unachotaka
kufanya.
Messi anaweza mpira, hilo halina ubishi lakini pia
hakuna ubishi anahitaji msaada wa kusonga mbele huku akiendelea kuwa na
mafanikio zaidi ya anayopata sasa na sehemu mbili zinazoweza kumsaidia ni yeye
na jamii.
Nyongeza, katika jamii kuna husuda, watu wengi
hawapendi wengine waendelee hata kama wao wanafanya juhudi. Usiseme nimesema
nina uhakika, ila kwa kuwa binadamu wanaishi ndani ya kikosi cha Simba, huenda
wako wanaomuonea husuda Messi na wanaweza kujaribu kutaka kumuangusha.
Nawashauri waache na badala yake wamsaidie kwa kuwa kwao anaweza kuwa rafiki,
ndugu au mdogo wao.
Maisha ni kusaidiana, ndiyo maana dunia ina watu wengi
kwa kuwa tunahitaji kushirikiana. Ukiona mwenzako anaonyesha njia ya mafanikio,
basi ungana naye umpe msaada kadiri ya uwezo wako. Kutaka kumrudisha nyuma, inawezekana
ni kujirudisha nyuma mwenyewe bila ya kujua. Wasalaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment