Na Saleh Ally
KILA kocha ana mfumo wake na anapopata timu ya
kuifundisha, daima imekuwa hivi, atafanya kitu ambacho lazima kitaonyesha kuna
tofauti na kocha aliyepita.
Mfano mzuri ni makocha wawili wapya, Zdravko Logarusic
wa Simba na Hans van Der Pluijm wa Yanga, ambao baada ya kuchukua timu,
waliingiza falsafa zao na kubadilisha mambo.
Logarusic aliyekabidhiwa timu kutoka kwa Abdallah
Kibadeni, aliona kuna ‘watoto’ wengi, kuna tatizo kwenye safu ya ulinzi na hadi
leo anasisitiza safu yake ya ushambuliaji haijakaa vizuri. Ndiyo maana
akamsajili kipa Ivo Mapunda na beki Donald Musoti.
Van Der Pluijm naye tayari amecheza mechi mbili za
kirafiki, mbili za mashindano akiwa na rekodi ya sare tatu na ushindi mmoja.
Lakini pia amefanya mabadiliko na hasa katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Juzi mara baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya
Coastal Union kwisha, van Der Pluijm aliwaambia waandishi wa habari mambo
mawili, kwamba pamoja na mchezo kuwa mgumu lakini kikosi chake kilishindwa
kufanya vizuri kutokana na uwanja mbovu na upepo mkali uwanjani hapo.
Huenda sababu hizo zimeonyesha kuwashangaza wengi
ingawa kweli kocha huyo ana haki ya kueleza kulingana na mwenyewe alivyoyaona
mambo katika mechi hiyo.
Mazungumzo yake yanalenga kujitetea kitu ambacho
makocha wengi hufanya, lakini kidogo inachanganya kwa kuwa siku chache tu
zilizopita baada ya mechi dhidi ya Ashanti, van Der Pluijm alisema hawakucheza
vizuri.
Mholanzi huyo alikiri kikosi chake hakikucheza vizuri
katika mechi dhidi ya Ashanti na akatoa sababu ya hali ya hewa, kwamba
walichelewa kuwasili nchini, hilo likachangia wao kutokuwa na pumzi ya kutosha.
Kukubali timu haikucheza vizuri na kuelezea kuhusiana
na suala la hali ya hewa ni kitu kilichokuwa ‘kinaingia akilini’, lakini hili
la upepo na uwanja, inawezekana van Der Pluijm inabidi afanye tathmini mara
mbili.
Kwa kuwa kama ni upepo, hiyo ni kawaida kwenye uwanja
huo na Yanga imecheza mara nyingi hapo. Lakini kuhusu uwanja, hapa ni tatizo
kwa kuwa si sahihi kusema Uwanja wa Mkwakwani ni mbaya, sehemu yake ya kuchezea
ni dhoofu kuliko Uwanja wa Bora au Loyola ambako wamekuwa wakifanyia mazoezi.
Labda ugeni pia wa Mholanzi huyo, bado hajui hali
halisi ya sehemu wanazofanyia mazoezi, lakini ukweli ulio wazi ni kwamba
hajapata kikosi sahihi na mabadiliko makubwa katika mechi mbili za ligi
alizocheza yanaonyesha.
Suala la kwamba hajapata kikosi anachotaka, linaweza
kukubalika hasa kwa kuwa ndiyo amejiunga na timu hiyo hivi karibuni.
Utaona katika mechi ya kwanza dhidi ya Ashanti, van
Der Pluijm alifanya mabadiliko ambayo hayakutarajiwa sana. Langoni alianza na
Deogratius Munishi ‘Dida’ badala ya Ally Mustapha ‘Barthez’ au Juma Kaseja,
kama ilivyotegemewa na wengi.
Beki wa kulia akamuanzisha Juma Abdul na kumchezesha
Mbuyu Twite namba nne, lakini akampa nafasi Said Bahanuzi kucheza namba kumi
huku akimtoa David Luhende kucheza beki hadi kiungo wa pembeni, kushoto.
Siku chache baadaye kwenye mechi ya Coastal, kikosi
cha kwanza akakifanyia mabadiliko makubwa matano, kumtoa Juma Abdul na nafasi
yake ikachukuliwa na Twite, halafu akamuingiza Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye
hakuwemo katika mechi ya Ashanti.
Kulia ambako alicheza Ngassa dhidi ya Ashanti,
akampanga Simon Msuva ambaye hakuanza mechi ya Ashanti, Ngassa amkabadilisha na
kumchezesha namba 10 ambayo alianza Bahanuzi katika mechi ya kwanza.
Mabadiliko hayo makubwa anayofanya van Der Pluijm,
yanaonyesha bado anasaka kikosi na huenda inaweza kuwa sababu ya msingi zaidi
kuliko upepo au hali ya uwanja.
Hata iwe vipi, lazima van Der Pluijm ajue kucheza
kulingana na mazingira ya sehemu halisi kwa kuwa kazi yake ni kuongoza kikosi
chake kupata ushindi na si vinginevyo.
Kweli, kuna tatizo la viwanja vya kuchezea, bado ni
duni, hii ni Afrika ingawa lazima wahusika wapambane nalo. Hivyo, van Der
Pluijm anatakiwa kulitambua mapema lakini si kuhusisha upepo kama kigezo cha
kucheza vibaya.
Inawezekana mara moja likakubalika, lakini haliwezi
kuwa utatuzi wa michezo mingine zaidi ya yeye kuhakikisha anakuwa na mbinu mbadala
kulingana na mazingira.
Kikosi Vs Ashanti:
Dida, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin
Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Said
Bahanuzi na David Luhende
Kikosi Vs Coastal:
Dida, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin
Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho
Ngassa na David Luhende.
0 COMMENTS:
Post a Comment