Timu ya JKT Oljoro inatarajia kuweka
kambi visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu
Bara unaotarajiwa kuanza Januari 25.
Oljoro kwa sasa inafundishwa na kocha
mpya, Hemed Morocco, baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Alex
Mwamgaya.
Morocco aliyeifundisha Coastal Union
katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kabla ya kutimuliwa, amesema
anadhani Zanzibar ni sehemu nzuri kwa ajili ya maandalizi.
Morocco alisema kuwa timu hiyo
itakapokuwa huko itacheza mechi mbalimbali za kirafiki ili kuweza kujiweka fiti
zaidi kabla ya mzunguko wa pili kuanza mapema mwezi huu.
“Tumeamua kwenda kuweka kambi
Zanzibar kwa muda mfupi uliobakia kwa ajili ya kujiimarisha zaidi kwa sababu
malengo yangu ni kuhakikisha timu yangu inatoka katika nafasi iliyopo kwa sasa
na kufikia nafasi za juu.
“Tukiwa huko tutacheza mechi
kama nne au tano ili kujiweka fiti, zaidi tutacheza na timu kama Mafunzo na
nyingine za huko kisiwani, lengo likiwa ni kujiimarisha zaidi,” alisema
Morocco.
Oljoro imemaliza mzunguko wa kwanza
wa Ligi Kuu Bara ikiwa katika nafasi ya 11 kwenye msimamo, baada ya
kujikusanyia pointi 10, sawa na Ashanti walio katika nafasi ya 12.
0 COMMENTS:
Post a Comment