MASHABIKI
wengi wa mpira hasa wale watu wenye tabia za kinazi au kikoma-ndoo, wamekuwa hawataki
kuambiwa ukweli hata kidogo.
Ikitokea
wameelezwa ukweli, wengi wao wamekuwa wakisingizia kitu kimoja tu, “umetumiwa”.
Yaani kama kuna kiongozi, mwanachama au shabiki wa klabu fulani na hasa Yanga
na Simba anaona umemueleza ukweli, utasikia anatumia lugha hiyo.
Neno
ametumika limekuwa la kawaida kabisa kwa wale wanaoshindwa kujibu hoja za
msingi kwa kuwa wanashindwa pa kusimamia, hivyo wanalazimisha kumaliza mambo
mapema ili wasijibu wanachotakiwa kufanya hivyo.
Katika
mkutano wa wanachama wa Yanga uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa PTA jijini Dar
es Salaam, kumejitokeza mambo kadhaa ambayo hakika yanaweza kuwa somo kwa
wapenda soka nchini.
Mwenyekiti
wa Yanga, Yusuf Mehbub Manji, alizungumza masuala kadhaa yanayohusiana na klabu
hiyo lakini kubwa lililowagusa na kuwakosha wengi ni kuhusiana na suala la
Katibu wa Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali.
Akilimali
anayejulikana na wapenda soka kama Abramovic, amekuwa mtu anayezungumza sana
kuhusiana na klabu hiyo, wakati mwingine kuitetea au hata kuvuruga mambo.
Wiki chache
zilizopita katika Hoja Yangu ya kila Ijumaa, nilizungumzia namna Mzee Akilimali
alivyozungumza kuhusiana na kipa Juma Kaseja akimsakama kwamba alichangia
kuifungisha Yanga katika mechi waliyofungwa 3-1 na Simba, na wao kama wazee
waliutaka uongozi kumsajili Ivo Mapunda na si yeye.
Nilieleza
kuhusiana na kila mmoja kumuachia nafasi mwenzake, kwanza haiingii akilini Mzee
Akilimali kuzungumzia masuala ya kiufundi au kuwashambulia wachezaji wake
hadharani, kitu ambacho si sahihi.
Lakini
jana, Manji amefunguka kwa staili yake ambayo naweza kusema ile tabia ya
kuamini ukiwa mtu mzima basi hata kama ukikosea haupaswi kuelezwa, si sahihi.
Manji
amemueleza Mzee Akilimali namna ambavyo amekuwa akiwakwaza, kama kiongozi wa
klabu akamueleza wanavyomheshimu, akasimulia namna mzee huyo alivyompokea
wakati anaingia Yanga, lakini mwisho akasisitiza suala la kuheshimu katiba.
Kauli ya
Manji hauwezi tena kuiita majungu, haikuwa na kunong’onezana wala kuitana
pembeni, badala yake kila kitu kimetokea mbele ya wanachama wote wa Yanga na
ninaweza kusema ilikuwa ni kwa njia njema ambayo huwezi kusema imemdhalilisha
Mzee Akilimali.
Kama ni
nidhamu haikuvunjwa na msisitizo wa Manji amesema anamheshimu sana, lakini
akasisitiza lazima katiba ifuatwe ambacho ni kitu cha msingi zaidi. Baada ya
hapo, Manji na Mzee Akilimali walipeana mikono na kukumbatiana.
Kilichonifurahisha
zaidi si wao kupeana mikono na kukumbatiana, badala yake ni namna Mzee
Akilimali alivyoamua kukaa kimya, kweli ameonyesha ni mzee hasa ambaye anajua
nini cha kufanya.
Hakukurupuka,
badala yake alikaa kimya. Naweza kusema ukimya wake umeonyesha ameelewa
alichoelezwa na yuko tayari kubadilika, pia ninaamini alichoelezwa ameamini ni kwa
manufaa ya klabu yao.
Kama Mzee
Akilimali amekubali kujifunza, suala la msingi ni kwamba kila mmoja ana nafasi
ya kujifunza na kukubali kwamba akikosea, akaelezwa basi ajirekebishe na suala
la “anatumiwa” au vinginevyo lisipewe nafasi.
Kama Mzee
Akilimali angekurupuka na kuamini Manji anamdhalilisha, au “anatumiwa” kama
ambavyo wamekuwa wakisema wengi wasiopima mambo, huenda asingeelewa somo
alilopewa. Lakini sasa atakuwa amepiga hatua moja mbele.
Ujasiri wa
Manji pia kumkosoa Mzee Akilimali ni jambo la kujifunza, tabia za woga wa
viongozi wengi kuonyesha hawajiamini na kuhofia kuonekana wabaya imechangia
klabu kongwe kuendelea kuyumba kwa kuwa uamuzi wa mambo, haufanyiki wakati
mwafaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment