Hodi Rage,
umewasikia Fifa na Okwi!
MAMBO
yamekuwa yakienda hatua kwa hatua na inawezekana kabisa baada ya muda mfupi
ujao ukweli wa kila kitu utakuwa hadharani kuhusiana na masuala ambayo nimekuwa
nikizungumzia juu ya suala la mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Hapa ni
haki bin haki, halafu hakuna woga kwa kuwa kinachozungumzwa ni ukweli mtupu na
aliye tayari anakaribishwa kwa ajili ya kujadili, waoga wa hoja mnaopenda kutoa
vitisho hapa si sehemu yenu, mimi leo naibuka tena na kupiga hodi kwa
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Huenda Rage
hakufanikiwa kusikia kuhusiana na suala la Okwi linavyoendelea, huenda amebanwa
na majukumu mengi kwa kuwa natambua ni Mbunge (CCM) wa Jimbo la Tabora Mjini,
huenda analazimika kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kulazimika kuyatimiza.
Pole sana
Rage kutokana na majukumu hayo, sijui kama unayaweza au kuyashindwa majukumu
hayo, siri yako moyoni lakini leo nataka kukukumbusha kuhusiana na suala la
Emmanuel Okwi ambalo awali uliwahi kusema mimi ni kasuku, leo hii hali taratibu
inakwenda inabadilika na huenda jina hilo lilikuwa sahihi kwako kama ambavyo
nilifafanua.
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuwa Okwi kwa sasa ni mali ya Yanga na
anaruhusiwa kucheza michuano ya ndani na ile ya kimataifa na atakuwa dimbani
kama akiwa fiti kuitumikia Yanga itakapokuwa ikitoana jasho na mabingwa wa
Afrika, Al Ahly.
Je, umesikia
au ulikuwa umebanwa na majukumu? Nilichokisema na wewe ukadai zilikuwa ni ndoto
au uchunguzi mbovu, taratibu kinaanza kutimia, kwamba wakati Simba ikiwa imemuuza
Okwi kwa dola 300,000 (Sh milioni 480) katika klabu ya Etoile du Sahel ya
Tunisia ikiwa haijapata hata senti, Fifa imesema anaweza kukipiga Yanga.
Okwi yuko
Yanga na Simba haijapata kitu! Nani anabisha, kati yako au wale waliokuunga
mkono kwa kujali urafiki wako au kuwa wapambe tu lakini hawakuangalia hoja za
msingi ambazo nilikuwa nazitoa kwako na wewe zikakuzidia ukaamua kuvurumisha
lawama lukuki na vitisho ukijaribu kunizima, kitu ambacho hakitakuwa na msamaha
kwa kuwa nitaendelea kusema ukweli hadi mwisho wa jambo hili, nasisitiza
sitakaa kimya hadi ukweli uwe hadharani na kama utakuwa sahihi, basi
nitakupongeza.
Hata kabla
Simba haijalipwa fedha zake, leo Okwi tayari amecheza katika vikosi vya klabu
tatu tofauti. Yaani Etoile ya Tunisia, SC Villa ya Uganda na sasa Yanga ya
Tanzania na Simba haijapata hata senti. Wewe ndiye ulifanya biashara hiyo na
hata Kamati ya Utendaji ya Simba ilisimama hadharani na kukukosoa kwamba
hukufuata utaratibu au hukwenda kama mlivyokubaliana hadi ikatangaza kukusimamisha.
Kuna wakati
nikakueleza kwamba Okwi sasa si mali ya Simba na unachotakiwa wewe ni kuweka
nguvu kudai fedha za Simba, ukakana, ukang’aka na kusisitiza Okwi hatakiwi
kucheza, hiyo haikuwa kazi yako, Okwi sasa kwa mujibu wa TFF ameidhinishwa
kucheza Yanga. Mimi naendelea kuhoji kuhusiana na malipo ya Okwi.
Kingine
ambacho kimenishangaza ni wewe kusema kwamba Etoile wameomba wasogezewe muda wa
kulipa deni hadi Septemba mwaka huu na wameomba hivyo kwa Fifa na Simba imepata
kopi. Sasa kama ni hivyo na wewe tayari ulisema hugombei, maana yake utawaachia
Simba deni hilo?
Nilifikiri
kama ungekuwa ‘smart’, basi ungejitahidi kuhakikisha Simba wanalipwa kabla ya wewe
kuondoka. Ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikisisitiza Okwi aliuzwa ‘bure’ kwa
kuwa Simba haikupata lolote licha ya kwamba siku chache kabla ya kumuuza, Simba
ilikuwa imemsainisha Okwi mkataba mpya na kumpa dola 40,000. Sijui unakumbuka! Maana nilikuona kwenye picha ukiwa
umetabasamu na Okwi akiwa karibu yako.
Nafikiri
huu ndiyo wakati mwafaka wa wewe wa kufunguka, waambie Wanasimba kwamba kama
Okwi anacheza Yanga, fedha za malipo yake vipi? Na kama umekubali Septemba na
wewe hutakuwepo vipi ufuatiliaji au umeamua kuliacha deni lisogee mbele ili
wakati wa uchaguzi useme unataka kugombea ili ushughulikie fedha za Okwi?
SOURCE: CHAMPIONI
saleh samahani ww mwenyewe huoni hapa kuna walakini sport club villa walilimnunua okwi kutoka timu ya tunisia au lipewa kwa mkopo mbona pesa wamepokea wao jamani huu ni ubaishaji
ReplyDeletemimi nafikiri tff hapa wametengeza kesi na hawakupeleka kesi fifa jinsi ilivyo, lakini yanga wakae wakijua hapa wanachezea sheria lakini yanga ndio tff lakini sio fifa
ReplyDeleteFIFA haijamruhusu Okwi kuchezea Yanga na imesema wazi kuwa hilo sio jukumu lao bali ni la TFF ambao wanatakiwa wazingatie article 5 juu uhamisho wa wachezaji. Kipengele hicho kiko rahisi tu mchezaji haruhusiwi kucheza msimu moja zaidi ya timu mbili na pia kama atahamia timu ya tatu basi asiwe na mgogoro wo wote wa kimkataba na timu zote mbili za awali. Wakati Okwi kipengele cha kucheza hakimbani bado anabanwa na kipengele cha mgogoro wa mkataba baina yake na timu yake ya kwanza. Lakini kwa sababu ya ushabiki wa katibu katoa tu maelekezo ya kukurupuka na itawagharimu. Kiutaratibu kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji ndiyo kilikuwa chombo sahihi cha kutoa tamko la juu ya majibu haya baada ya kuipitia barua ya FIFA. Lakini tumeyazoea haya na wewe mwandishi unayashabikia badala ya kusaidia kurekebisha. Shafih Dauda kayaweka vizuri tena kwa vielelezo vizuri lakini TFF watajifanya hawaoni.
ReplyDelete