Na
Saleh Ally
APRILI
2, 2009, Yanga ilifungwa bao 1-0 na wageni wao, Al Ahly, katika mechi ya kwanza
ya Ligi ya Mabingwa, mechi ambayo huenda Yanga walikuwa na nafasi kubwa ya
kushinda lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika umaliziaji.
Wakenya,
Boniface Ambani na Mike Barasa, walikuwa na nafasi ya kufunga zaidi ya mabao
mawili, lakini nafasi nyingi zilipotelea miguuni mwao baada ya kupata pasi
nzuri huku kila mtu akiamini walikuwa wanatikisa nyavu.
Yanga
inashuka dimbani Machi Mosi au 2, kuwavaa tena Al Ahly ambao ni mabingwa wa
Afrika, mechi inayotarajiwa kuwa nzuri kwa kuwa Yanga haina sababu kuwa na woga
kwa Waarabu hao wa Misri, lakini lazima ikubali kuwa jamaa wanajua na wana
uzoefu mkubwa na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kivutio
katika mechi hiyo ni kutokana na mechi ya mwisho iliyozikutanisha timu hizo
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mechi inayofuatia, kuna mambo
kadhaa ya kujifunza.
Nyumbani:
Timu
hizo katika ligi za nyumbani zinaonekana kutokuwa na tofauti sana ingawa Al
Ahly inaonekana kusuasua zaidi ya Yanga. Kwani katika mechi tatu zilizopita,
kikosi cha kocha Hans van Der Pluijm kimeshinda mbili dhidi ya Ashanti United
(2-1), sare ya bila kufungana na Coastal Union halafu kikawapiga Mbeya City
(1-0).
Kwa
Al Ahly katika ligi ya Misri mechi hizo tatu, imepoteza moja, sare moja na
kushinda moja. Ikiwa nyumbani iliishinda Ghaz El Mehalla kwa bao 1-0, ikabaki
nyumbani na kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Al Ittihad kabla ya
kukiona cha moto juzi Jumamosi kwa kuchapwa 1-0 ugenini dhidi ya El Gounah.
Ukizungumzia
kwa rekodi ya nyumbani, Yanga wanayo nzuri, lakini bado si kipimo cha mwisho
cha ubora wa timu hizo zitakapokutana jijini Dar es Salaam, takribani wiki
mbili tu zijazo.
Vikosi:
Kuna
rekodi kwenye kikosi cha Yanga kilichokutana na Al Ahly na ambacho kitacheza
nayo tena wiki mbili zijazo kwa kuwa kuna wachezaji walikuwepo Yanga tokea
wakati huo na walicheza na sasa bado wapo.
Kipa
Juma Kaseja, ndiye alikuwa langoni siku hiyo wakati Flavio Amado raia wa Angola
alipofunga bao pekee la mechi baada ya kupokea pasi ya Mohamed Aboutrika.
Lakini Kaseja aliondoka na kujiunga na Simba, kabla ya kurejea tena Yanga msimu
huu.
Beki
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwepo tokea wakati huo, katikati alisimama na
George Owino. Mrisho Ngassa pia alicheza dakika zote 90, bado yuko Yanga lakini
aliondoka na kujiunga na Azam FC, Simba kabla ya kurejea Yanga msimu huu.
Mkongwe
Athumani Idd ‘Chuji’, alicheza dakika zote 90, kocha Dusan Kondic akimpanga
namba 11. Mchezaji wa tano ambaye anakutana na Al Ahly tena ni Jerry Tegete,
siku hiyo alianzia benchi kabla ya kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya
Boniface Ambani ambaye siku hiyo ‘alichemsha’.
Makocha:
Makocha
kwa kila upande ni wageni, wakati Al Ahly inafundishwa na mzalendo Mohammed
Yosseuf, kipindi hicho ilipokuja Dar es Salaam ilikuwa chini ya Kocha Mreno,
Manuel Jose. Yanga ilikuwa na Mserbia, Dusan Kondic aliyekuwa akisaidiwa na
Mcroatia Spaso Skolosovosk na Mserbia mwingine, Civojnov Serdan, sasa ina
Mholanzi van Der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
Rekodi
dhidi yao:
Ukizungumzia
rekodi ya timu hizo kukutana, tokea mwaka 1982 inaonyesha timu hizo zimekutana
mara tatu. Wakati huo ikijulikana kama Klabu Bingwa Afrika, mara ya kwanza
mwaka huo, Al Ahly iliishindilia Yanga mabao 5-0, waliporudiana jijini Dar es
Salaam ikawa sare ya bao 1-1.
Mara
ya pili ilikuwa mwaka Aprili 9, 1988, Yanga ilikomaa na kupata sare ya bila
kufungana, Aprili 22 ilikuwa jijini Cairo ambako ilikutana na kipigo cha mabao
4-0.
Mechi
ya tatu ni mwaka 2009, mechi ya kwanza Yanga ililala kwa mabao 3-0 nchini Cairo
na iliporudi hapa jijini Dar es Salaam ikalala kwa bao 1-0 na mabingwa hao wa
Afrika wakati huo wakasonga mbele na jumla ya mabao 4-0.
Wengine:
Al
Ahly imekuwa mbabe wa timu za Tanzania na si Yanga pekee, rekodi zinaonyesha
mwaka 1985, Simba ilijitutumua na kuichapa Al Ahly kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba, Mwanza, hii ilikuwa ni michuano ya Kombe la Washindi wakati
huo, lakini ilipofunga safari kwenda Cairo, ikafungwa mabao 2-0 na kutoka.
Mwaka
1993 katika Kombe la Washindi tena, Al Ahly ikakutana na timu nyingine ya
Tanzania, ilikuwa zamu ya Pamba ya Mwanza na mechi ya kwanza Cairo, Pamba
ikalala 5-0 mjini Mwanza, kwenye marudiano ikawa sare ya bila kufungana.
Timu
nyingine iliyowahi kuingia katika anga za Al Ahly ambayo si Yanga au Simba ni
Majimaji ya Songea, ilikuwa mwaka 1999. Mechi kwenye Uwanja wa Taifa ‘Shamba la
Bibi’, Majimaji ililala kwa mabao 3-0
halafu ikafungwa tena 2-0 jijini Cairo.
0 COMMENTS:
Post a Comment